HOTUBA YA MHE. SOPHIA M. SIMBA (MB),
Kwanza, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru mwenyezi
mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha sote kukutana hapa ili kuweza
kushuhudia tukio hili muhimu katika kuwezesha watoto kupata mojawapo
ya haki yao ya msingi.
Ndugu Wageni Waalikwa
Mnamo mwaka 2009 Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia
na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya watoto
hapa nchini ilifanya utafiti wa kina ili kufahamu ukubwa na sura ya
ukatili wa kijinsia, kimwili na kiakili yanayowasibu wasichana na wavulana
hapa nchini. Utafiti huu ulifanywa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu
cha Afya ya Sayansi na Tiba cha Muhimbili (Muhimbili University of Health
and Allied Sciences – MUHAS) kwa kushirikiana na UNICEF na Kituo cha
Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Center for Diseases Control – CDC).
Ripoti ya Utafiti huu ilizinduliwa rasmi mnamo tarehe 09 Agosti, 2011
na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa bibi Asha-Rose Migiro.
Matokeo ya utafiti huu yalionyesha kuwa kuna kiwango
kikubwa cha ukatili dhidi ya watoto na matukio mengi ya ukatili kwa
watoto yamekuwa yakifanyika ama shuleni na au nyumbani. Hali hii
ilipelekea wadau wa masuala ya watoto (Taasisi za serikali na zile zisizokuwa
za serikali) kuandaa Mpango Mkakati wa mwaka mmoja wa Kushughulikia
Tatizo la Ukatili Dhidi ya Watoto (2012 – 2013) na hatimaye kuandaa
Mpango wa miaka mitatu wa kushughulikia tatizo hilo (2013 – 2016)
ambao ulizinduliwa mwezi April mwaka huu.
Ndugu Wageni Waalikwa
Mnamo tarehe 3 Januari, 2013
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto iliingia makubaliano
na Asasi Isiyokuwa ya Kiserikali ya C-Sema kuhusu uendeshaji wa mtandao
huu katika maeneo ya majaribio (Pilot Areas). Uendeshaji wa mtandao
huu katika maeneo haya utasaidia kutoa picha halisi ya namna nzuri ya
uendeshaji wa mtandao wa namna hii hapa nchini. Mtandao huu utafanya
kazi katika Wilaya/ Manispaa za Temeke, Magu, Bukoba Vijijini, Musoma
Mjini, Kasulu na Hai ambapo muda si mrefu utaanza kufanya kazi katika
Manispaa za Ilala na Kinondoni. Lengo kuu la Serikali kwa kushirikiana
na wadau wake wa maendeleo ya watoto ni kuhakikisha kuwa mtandao huu
unafanya kazi katika maeneo yote ya Tanzania Bara.
Ndugu Wageni Waalikwa
Uanzishaji wa Mtandao wa Mawasiliano wa Kusaidia
Watoto ni moja wapo ya shughuli ambazo zilipangwa kutekelezwa na Wizara
yangu katika Mpango wa Miaka Mitatu wa Kushughulikia Ukatili Dhidi
ya Watoto uliozinduliwa hivi karibuni. Kadhalika, ni moja wapo ya utekelezaji
wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watoto (The UN Convention
on the Rights of the Child – UN CRC) ambao nchi yetu iliusaini na
kuuridhia mara baada ya kupitishwa kwake. Mtandao huu utatoa fursa kwa
watoto na au watu wazima kwa niaba ya watoto kutoa taarifa za ukatili
unaofanywa kwa watoto katika eneo fulani ili kuwezesha wahusika kufuatilia
kwa karibu na urahisi kwa ajili ya kutoa msaada kwa mtoto/watoto waliofanyiwa
vitendo vya ukatili na kumchukulia/kuwachukulia hatua mhusika/wahusika
wa vitendo hivyo vya ukatili. Kwa kiasi kikubwa kama mtandao utatumiwa
kwa malengo haya, ni imani yangu kuwa itasaidia kupunguza ukatili dhidi
ya watoto na vile vile kuhakikisha kuwa watoto wanapata msaada stahiki
kwa wakati.
Ndugu Wageni Waalikwa
Ni matumaini ya Wizara yangu kuwa wadau mbalimbali
watajitokeza kushirikiana nasi katika kuhakikisha kuwa huduma hii inapatikana
katika maeneo yote hapa nchini katika muda muafaka ili kuhakikisha kuwa
watoto wetu wanapata ulinzi wa kutosha. Kadhalika, ni matumaini yangu
kuwa jamii na wahusika wote watawezeshwa kupata uelewa wa kutosha kuhusu
matumizi sahihi ya mtandao huu.
Mwisho, napenda pia kuchukua fursa hii rasmi kutamka kuwa
nimezindua rasmi mtandao wa mawasiliano ya simu wa kusaidia watoto katika
maeneo ya majaribio niliyoyataja hapo mwanzo.
Tuungane kwa Pamoja Kuijenga Tanzania Imfaayo Mtoto.
MWANA HARAKATI