Akitoa matokeo ya awali ya utafiti
huo, mmoja wa watafiti wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha
Muhimbili, kitengo cha magonjwa na afya ya akili, Lusajo Kajula, alisema kuwa
asilimia 10 ya vijana wenye umri wa miaka 12 hadi 14 ambao ni wanafunzi wa
darasa la tano na sita wameshawahi kufanya ngono.
Alisema ngono hiyo kwa asilimia
kubwa hufanywa na wanafunzi hao kinyume na maumbile.
Kajula alisema vijana wengi
wamebainika kufanya ngono ya kawaida na ya mdomo, ikifuatiwa na ngono ya
kinyume na maumbile.
Alisema kwa wale ambao wameshawahi
kufanya ngono, asilimia 6.3 wamefanya kinyume na maumbile wakati asilimia 93.7
hawajawahi kufanya.
Alisema utumiaji wa kondomu
umebainika kuwa mdogo kwa vijana wadogo ambao wameanza kufanya ngono.
“Asilimia 68 ya wale walioanza
kufanya ngono hawajawahi kutumia kondomu kabisa, wakati asilimia 32 wamewahi
kutumia,” alisema.
Alisema hiyo ni sehemu ya utafiti wa
miaka minne ulioshirikisha Chuo Kikuu cha Makerere cha Uganda, Cape Town na
Limpopo vya Afrika Kusini, Bergen na Oslo vya Norway, Maastricht cha Uholanzi
na Sussex cha Uingereza.
Katika utekelezaji wa utafiti huo,
wanafunzi 5,099 walichaguliwa mwanzoni mwa mradi kufanyiwa utafiti huo, ambapo
4,783 (asilimia 93.9) walifuatiliwa kwa miezi 6 na wengine 4,370 (asilimia
85.8) kwa miezi 12.
Mradi huo wa PREPARE ulitekelezwa
kwenye shule 38 kutoka Manispaa ya Kinondoni zilizochaguliwa, kwa kutumia
sampuli mtawanyiko, zilizopangwa katika makundi mawili ya shule.
“Kimsingi tunataka kuwaambia wanahabari
kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa ya mradi wa PREPARE ni kuchelewesha kuanza
ngono miongoni mwa wanafunzi wa kiume na wa kike wenye umri wa miaka 12-14
katika Mkoa wa Dar es Salaam,” alisema Kajula.
Matokeo yaliyotathminiwa ni
mabadiliko katika masuala ya ngono (kuanza ngono) na kutumia kondomu wakati
wa kujamiiana kwa wale waliokwishaanza vitendo hivyo.
Kajula alisema kwa wastani mradi wa
PREPARE umefanikiwa kupunguza uwezekano wa vijana wadogo hasa wavulana na
wasichana kuanza ngono na kuongeza matumizi ya kondomu kwa wale walioanza.
Hata hivyo, katika utekelezaji wa
mradi mabadiliko katika uchukuaji wa hatua yalionekana zaidi miongoni mwa
wasichana waliopata mwingilio ukilinganisha na wale ambao hawakupata.
Alisema uchukuaji wa hatua ulisababisha
kuwapo tabia ya kutumia kondomu kwa wanafunzi wa jinsia zote na taarifa za
ongezeko la utumiaji wa kondomu miongoni mwa vijana wa kiume.
Kajula alisema ili kuweza kupata
matokeo yaliyokusudiwa, mradi ulitoa mafunzo kwa walimu watano wakufunzi wa
wakufunzi.
Alisema mradi ulitoa mafunzo kwa
walimu watekelezaji 76, na waelimishaji rika wanafunzi 132 na kuelekeza
watoa huduma 8 wa afya katika kliniki za huduma rafiki kwa vijana ili
kutekeleza mwingiliano.
Mradi huo umefadhiliwa na Umoja wa
Nchi za Ulaya, ambapo programu ya utafiti wa afya imelenga kuangalia mwingilio
ulio katika misingi ya utamaduni na jinsia, endelevu, kijamii ili kukuza
ujinsia na afya ya uzazi miongoni mwa vijana wenye umri miaka 12-14 kwa kutumia
shule kama njia ya kufundishia.
Mtathmini kiongozi wa mradi huo,
Mrema Kilonzo, alisema utafiti umeonyesha haja ya kutolewa elimu ya afya ya
uzazi kwa vijana wadogo ambao bado hawajaanza ngono ili kuchelewesha kuanza
ngono kwa mfumo wa kisaikolojia kama njia ya kufanya wajitambue.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment