MAC PRODUCTION STUDIO'S

MAC PRODUCTION STUDIO'S
KWA MATANGAZO YA BIASHARA REDIONI( 0767-814844)

Monday 29 April 2013

MABADILIKO YA KATIBA


Na Mwandishi Wetu

Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesema imejipanga kuandaa rasimu ya katiba itakayoweka mbele maslahi ya taifa na kuwaomba wananchi waijadili na kutoa maoni yao katika mabaraza ya katiba yatakayokutana kuanzia mwezi Juni mwaka huu (2013).

Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Jospeh Warioba amesema leo (Jumatatu, Aprili 29, 2013) jijini Dar es Salaam kuwa katika kuandaa rasimu hiyo, Tume yake haitapokea shinikizo kutoka taasisi, asasi, makundi au vyama vya siasa.

“Tume haitengenezi katiba ya vikundi au vyama, tunaandaa katiba ya nchi,” amesema Jaji Warioba katika mkutano wake na waandishi wa habari katika ofisi za Tume na kufafanua kuwa Tume inazingatia uzito wa hoja zilizotolewa  na wananchi na sio idadi ya watu waliotoa maoni.

Jaji Warioba amewataka wananchi kutokubali kutumiwa na makundi, asasi, taasisi na vyama wakati wa kujadili na kutoa maoni katika mabaraza ya katiba ya wilaya.

Mabaraza ya Wananchi wenye ulemavu
Akizungumza kuhusu ushiriki wa walemavu katika mabaraza ya katiba, Jaji Warioba amesema Tume yake inatarajia kuunda mabaraza ya Katiba ya watu wenye ulemavu ili kuwapa fursa walemavu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa na Tume.

Hatua hii inafuatia ombi la Shirikisho la Vyama vya Watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) na Umoja wa Watu wenye ulemavu Zanzibar (UWAZA) waliloliwasilisha kwa Tume.

Jaji Warioba amesema Baraza moja litaundwa Tanzania Bara na jingine Zanzibar na kwamba yatashirikisha wananchi kutoka ngazi ya chini ya wilaya hadi Taifa.

“Tunaelewa kuwa watu wenye ulemavu ni karibu asilimia 10 ya watanzania wote na mchakato huu hauwezi kuwatenga katika ngazi yoyote,” amesema Jaji Warioba na kuongeza kuwa taarifa ambazo Tume yake inazo zinaonyesha baadhi ya watu wenye ulemavu wamependekezwa na mitaa, vijiji, vitongoji na shehia kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.

Aina na Majukumu ya Mabaraza ya Katiba
Katika mkutano huo uliofanyika katika katika Ofisi za Tume zilizopo mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti huyo pia alizungumza kuhusu aina na majukumu ya Mabaraza ya Katiba.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 imetoa fursa ya kuundwa kwa mabaraza ya aina mbili ambayo ni Mabaraza yatakayoundwa, kusimamiwa na kuendeshwa na Tume katika muda na tarehe itakayopangwa na Tume.

Aina ya pili, kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, ni Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi mbalimbali yenye malengo yanayofanana. Mabaraza haya yatajiunda, yatajisimamia na kujiendesha yenyewe na kisha kuwasilisha maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba ndani ya muda utakaopangwa na Tume.

“Kazi kubwa ya Mabaraza ya Katiba ya aina zote mbili ni kuipitia, kuijadili na kuitolea maoni rasimu ya Katiba itakayokuwa imeandaliwa na Tume kutokana na maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wananchi,” alisema Jaji Warioba na kuziomba taasisi, makundi, asasi na vyama mbalimbali kutumia fursa hiyo ya kisheria kuunda mabaraza na kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa.
MWANA HARAKATI

MKUU WA MKOA WA KAGERA AMEOMBA USHIRIKIANO KWA VYOMBO VYA HABARI KUHAMASISHA KUHUSU SIKU YA MASHUJAA 2013

Mkuu wa mkoa wa KAGERA, Kanali mstaafu FABIAN MASSAWE, ameshauri vyombo vya habari na Wana habari kuhamasisha jamii mkoani humo kujiandaa kikamilifu  kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa.
Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa  hufanyika  kila tarehe 25 mwezi Julai. Kitaifa mwaka huu  yatafanyika Julai 25, mkoani KAGERA, katika kambi ya Jeshi la Wananchi-JWTZ-KABOYA, wilayani MULEBA.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo  atakuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk JAKAYA KIKWETE.

Kanali MASSAWE amesema  vyombo vya habari na Wanahabari  ni kiungo muhimu katika kuhamasisha jamii iweze kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo.

Ameshauri Wazee walioshiriki matukio  wakati ule kujitokeza na kusimulia  ili liwe fundisho kwa   jamii ya sasa itambue uzalemdo wa kuipigania nchi yao.

Aidha, amewataka Wakazi wa mkoa wa KAGERA kutumia fursa hiyo kuwekeza zaidi na kupata ajira.
 Picha juu na nichi ni baadhi ya waandishi habari wa vyombo mbalimbali wakifuatilia katika mkutano huo uliowashirikisha wadau wa habari pia.
MWANA HARAKATI

MBUNGE WA ARUSHA MJINI AMEACHILIWA KWA DHAMANA

MBUNGE wa jimbo la Arusha mjini Godbles Lema ameachiwa kwa dhamana hadi tarehe 29 mwezi wa tano kesi hiyo itakapotajwa tena katika Mahakamana hiyo.


Baada ya Mbunge huyo kuachiliwa huru, umati wa wanachama wa Chadema waliokuwa wamejazana katika Mahakama hiyo walifanya maandamano makubwa kwenda katika Ofisi za Chama hicho zilizopo maeneo ya Ngarenaro.

Mbunge huyo amekutwa na makosa matatu ambapo kosa la kwanza ni kuwaambia wanafunzi wa chuo cha uhasibu alipoenda kuwatuliza kuwa ‘dhambi kubwa kuliko zote ni woga ‘.Haki hutafutwa na kupiganiwa ikiwa jambo unalipigania ni la msingi na linafaa kupiganiwa.

Kosa la pili ni pale alipotamka kuwa “Tumemtafuta mkuu wa mkoa juu ya Matatizo yenu na mlivyoshuhudia hapa amechukua muda mrefu na kuingia kama vile anaingia kwenye send-off.
Kosa la tatu ni pale alipotamka kwa wanafunzi kuwa “Mimi Mbunge wenu nipo sambamba nanyi hadi mpate haki yenu na ikiwa mkuu wa Mkuu wa Mkoa hatakuja hapa kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi wa mkoa nitawaongoza hadi ofisini kwake ili mpate majibu na haki yenu kwani ni haki yenu ya msingi kwa mujibu wa katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ambayo niliapa kuilinda Bungeni na pia inaruhusiwa kwa mujibu wa kikanuni na kifalsafa katika utekelezaji wa utawala bora wa kidemokrasia ambao msingi wake ni kusikilizwa na kulinda haki za binadamu’’.
MWANA HARAKATI