Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za vifo vya wachezaji watano wa
timu ya Rusumo FC ya mkoani Kagera vilivyotokea jana jioni (Oktoba 16 mwaka
huu).
Rusumo FC ilikuwa ikitoka
kwenye mechi ya michuano ya Polisi Jamii Wilaya ya Ngara ambapo ikiwa njiani
kurudi Rusumo kutoka mjini Ngara ilipata ajali ya gari na wachezaji watano
kufariki papo hapo. Wachezaji wengine ambao ni majeruhi wamelazwa Hospitali ya
Wilaya ya Ngara ya Murugwanza huku wawili hali zao zikiwa mbaya.
Msiba huo ni pigo kwa familia
za marehemu, klabu ya Rusumo FC, Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ngara
(NDFA), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera (KRFA) na familia ya mpira wa
miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango wa wachezaji hao katika ustawi wa
mchezo huu kupitia klabu yao.
TFF inatoa pole kwa familia za
marehemu, Rusumo FC, NDFA na KRFA na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi
hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Kutokana na msiba huo, mechi
zote za Ligi Kuu ya Vodacom zinazochezwa leo (Oktoba 17 mwaka huu) kutakuwa na
dakika moja ya maombolezo ili kutoa heshima kwa marehemu hao. Mungu aziweke
roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.
KIM, KUSHUHUDIA MECHI ZA LIGI
KUU Z’BAR Kocha Mkuu wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen wikiendi hii
ataanza ziara ya Zanzibar kuangalia Ligi Kuu ya Grand Malta kuwania ubingwa wa
Zanzibar. Kim anatarajia kushuhudia mechi zilizopungua tano akianzia kisiwani
Pemba ambapo kati ya Oktoba 19 na 21 atashuhudiwa mechi mbili zitakazochezwa
kwenye Uwanja wa Gombani.
Mechi hizo ni kati ya mabingwa
watetezi wa Ligi Kuu ya Grand Malta, Super Falcon ambao watacheza na vinara wa
ligi hiyo Bandari, na baadaye mechi kati ya Duma na Bandari.
Baadaye atakwenda Unguja kwenye
Uwanja wa Amaan ambapo baadhi ya mechi alizopanga kushuhudia ni kati ya Mtende
na Chipukizi, Mundu na Jamhuri na KMKM dhidi ya Zimamoto. Boniface Wambura
Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Taarifa hii ni kwa hisani ya MJENGWA BLOG.
No comments:
Post a Comment