Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Ernest Mangu ametoa tamko hilo hii leo ofisini kwake.
Amesema kwamba tayari jeshi hilo limetoa taarifa kwa Askari wa Interpol na Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini Dar es salaam ili kusaidia kuwakamata na kuwarejesha watuhumiwa wawili ambao ni viongozi wa Kidini wanatuhumiwa kwa kutoa Kanda (DVD na CD) zilizo na maudhui ya uchochezi wa kiimani kwa madhehebu ya Kidini nchini. (ZAIDI OFYA PLAY MSIKILIZE)

“Tangu mwezi wa Februari mwaka huu
tulitoa rai ya kuwatafuta watu watatu ambao ni viongozi wa kidini kwa tuhuma
hizi za uchochezi lakini hadi sasa tumefanikiwa kumkamata mmoja wao aitwaye
Imamu Hamza Omary na kumfungulia mashitaka huku yukiwa tayari tumeisha mfikisha
katika mahakama ya Wilaya kuendelea na kesi”alisema Kamanda.
Kamanda Mangu amewataja watuhumiwa wengine wanaotafutwa na jeshi hilo na wanaodaiwa kutoroka nchini kwa ni Sheikh Ilunga Hassan Kapungu kiongozi wa Taasisi ya kidini ya Thaqeeb iliyopo Kata ya Nyamanoro Wilayani Ilemela na Askofu Augustine Mpemba wa Kanisa la Tanzania Field Evangelist na Mkurugenzi anayemiliki kituo cha Redio Kwa Neema FM cha Jijini Mwanza ambacho kimefungiwa na TCRA miezi sita kwa ukiukwaji wa maadili.
“Hawa wawili tumeamua kuwashirikisha
polisi wa Interpol ili kuwakamata na kuwarejesha nchini ili kuwaunganisha na
kesi tuliyomfungulia mwenzao Imamu Omary na tunasikia kuwepo kwa taarifa kuwa
Sheikh Ilunga kuwa yupo nchini India na Askofu Mpemba yupo nchini Marekani
wanakodaiwa kutorokea,bado tutahakikisha tunawakamata tu ni vyema
wakajisalimisha kabla ya hawajakamatwa ”alisisitiza.
Kamanda Mangu ametoa muda wa siku nne kwa
wafanyabiashara wanaouza na kusambaza Kanda (DVD na CD) za uchochezi
ziliotolewa na watuhumiwa hao wanaotafutwa na jeshi hilo na zingine
zenye maudhui ya uchochezi wa kiimani wa kidini kuzisalimisha kwa ihali yao
kwenye vituo vya polisi kabla ya kuanza opresheni ya kuzisaka Jijini
Mwanza na Wilaya zote za Mkoa huo na hata ile ya jirani.
Kanda zilizopigwa marufuku ni pamoja
na Unafiki katika Sensa, Bakwata tawi la Kanisa,Mauaji ya
Sheikh Abdu Rogo wa Mombasa na Mwisilamu rudisha Imani zilitolewa na
Sheikh Ilunga, Ndege wote walie akilia Bundi Uchuro ya Imamu
Omary na Inuka chinja ule iliyotolewa na kusambazwa na Askofu
Mpemba.
Wito umetolewa kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za siri kwa jeshi hilo ili kuweza kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na watu wanaoendelea kusambaza na kuziuza kanda hizo kwa usiri ili kuwafikisha katika chombo cha sheria kutokana na kueneza uchochezi wa kiimani ka madhehebu ya kidini jambo ambalo linahatarisha amani ya nchi na huweza kusababisha machafuko zaidi ya kidini.
No comments:
Post a Comment