Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete ameitaka Jumuia ya Kimataifa kufanya kila linalowezekana kumaliza
mzozo wa kisiasa na mapigano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ili kutoa nafasi
kwa wananchi wa Congo kuishi katika amani na kujitafutia maendeleo.
“Hawa ni
watu walioteseka sana na kwa muda mrefu, wana haki ya kupata amani,
wana haki ya kupata muda wa kupumzika kutokana na vita na mapigano,” Rais Kikwete ameuambia mkutano wa pili wa wakuu wa
nchi zilizotia saini mkataba wa kutafuta amani, usalama na ushirikiano
katika DRC chini ya Umoja wa
Mataifa (UN).
Katika mkutano huo, uliofanyika leo, Jumatatu, Septemba
23, 2013, kwenye Umoja wa Mataifa mjini New York chini ya Uenyekiti
wa Katibu Mkuu wa UN, Mheshimiwa Ban Ki
Moon kama ulivyokuwa mkutano wa kwanza uliofanyika Februari 24, mwaka
huu, 2013, mjini Addis Ababa, Ethiopia, Rais Kikwete amewaambia viongozi
wenzake wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) na wengine waliotia
saini mkataba huo:
“Nadhani
hatua zilizochukuliwa mpaka sasa kuhusu DRC ni nzuri na mchakato wa
kutafuta amani nchini humo unakwenda vizuri. Ni muhimu tukafikia mwisho
wa tatizo hili kwa sababu wananchi wa DRC wametesema mno na kwa muda
mrefu. Wana haki ya kupata amani, wana haki ya kupata muda wa kutosha
wa kufanya mambo ya maana kama ya maendeleo yao badala ya kukaa na kufikiria
vita,” Rais Kikwete amesema kwenye mkutano huo.
Rais Kikwete amesema kuwa siri ya kufanikiwa katika
DRC ni kutekeleza yale yote ambayo nchi hizo zimekubaliana kutekeleza
katika DRC akisisitiza: “La msingi
ni kila mmoja wetu kutekeleza yale yote tuliyokubaliana. Hiyo ndiyo
siri ya kuleta amani na utulivu katika DRC.”
Mbali na Rais Kikwete, mkutano huo wa leo umehudhuriwa
na Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye pia ni Mwenyekiti wa ICGLR, Rais Jacob Zuma
wa Afrika Kusini, Rais Joseph Kabila Kabange wa DRC, Rais Paul Kagame
wa Rwanda, Rais Joyce Banda wa Malawi ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuia
ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mwenyekiti wa
Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Mheshimiwa Nkosazana
Dlamini-Zuma, na Katibu Mkuu wa UN ambaye alikuwa mwenyekiti
wa mkutano huo.
Aidha, mkutano huo umehudhuriwa na Makamu wa Rais
na wawakilishi wa Jamhuri ya Congo (Congo-Brazzaville), Zambia, Angola
na Sudan Kusini.
Kwenye mkutano huo, wasemaji wengi wamesisitiza kuwa
hakuna amani ya kweli katika DRC na nchi za Maziwa Wakuu bila viongozi
wa nchi hizo kukubali kuzungumza na kukubaliana na vikundi mbali mbali
ambavyo vinapigana dhidi ya baadhi ya nchi hizo.
Baadaye leo, Rais Kikwete amehudhuria mkutano wa Baraza la Uongozi la Umoja
wa Kutafuta Usalama wa Chakula na Ushirikiano wa Grow Africa uliofanyika
kwenye Ofisi za Taasisi ya Uchumi Duniani (WEF) uliofanyika kwenye ofisi
za taasisi hiyo katika Marekani mjini New York.
Rais alizungumza kwa ufupi katika mkutano huo ambako
alitaka wafadhili wa miradi ya kilimo katika Afrika kuongeza kasi ya
kutoa fedha za kuleta mageuzi ya kilimo katika Bara la Afrika kwa sababu
kila mmoja wa wadau anatekeleza majukumu yake kwa haraka zaidi kuliko
wafadhili.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais,
Ikulu,
MWANA HARAKATI
No comments:
Post a Comment