Watu wawili wamekufa
katika matukio tofauti wilayani Bunda, mkoani Mara, akiwemo mwanamke mmoja
aliyeuawa na mchumba wake na kufukia mwili wake porini na kisha fisi kufukua
kaburi hilo na kichwa chake kuonekana mitaani kikiliwa na mbwa.
Tukio hilo la
kikatili lililothibitishwa na polisi, limetokea Machi 22 mwaka huu, majira ya
saa 3:00 asubuhi katika kijiji cha kiroreli wilayani Bunda.
Mwanamke aliyeuawa
na mchumba wake ametambuliwa kwa jina la Wambura Magonze, mkazi wa kijiji cha
Kiroreli.
Polisi wamesema kuwa
baada ya kupata taarifa ya tukio hilo walikwenda katika eneo la tukio
wakiongozana na mkuu wa upelelezi wilayani hapa, Munguwajuna, na kukuta mbwa
mitaani wakila kichwa cha marehemu huyo.
Imeelezwa kuwa
mwaume huyo baada ya kumuua mchumba wake kwa kipigo, wakiwa wanatoka shambani
aliuzika mwili wake porini katika kaburi lenye urefu wa futi moja.
Aidha, imeelezwa
kuwa baadaye wanyama wanaodhaniwa kuwa ni fisi waliufukua mwili huo na kuanza
kuula, na kwamba kichwa cha marehemu kilionekana mitaani kikiliwa na mbwa.
Mwanaume huyo Matoka
Maroba Isumail (24) mkazi wa kijiji hicho, baada ya tukio hilo alitoroka,
lakini baadaye akakamatwa na polisi na amekiri kufanya mauwaji hayo.
Polisi wamesema kuwa
awali mwanaume huyo aliandika ujumbe kwenye vipande vya karatasi vipatavyo saba
na kuvipeleka nyumbani kwa baba wa mwanamke huyo, ambavyo vilikuwa na vitisho
kadhaa.
Katika maelezo yake
aliyotoa polisi mwanaume huyo amesema kuwa aliamua kumuua mchumba wake huyo kwa
sababu baba yake alikuwa anataka kumuoza kwa mume mwingine kwa mahali nyingi,
licha ya yeye kukubaliana kutoa mahali ya ng’ombe saba na laiki sita, pamoja na
kutoa kishika uchumba cha sh. 70,000.
Ameongeza kuwa baada
ya kumuua mchumba wake yeye pia alikuwa anao mpango wa kujiua na kwamba tayari
alikuwa amekwishaandika historia ya maisha yake ambayo ingesomwa wakati wa
mazishi yake.
Mtuhumiwa huyo
leo Jumatano amefikishwa kwa mlinzi wa amani na akakiri kufanya mauaji hayo,
ambapo kesho asubuhi atafikishwa katika mahakama ya wilaya ya Bunda, kujibu
tuhuma hiyo.
Na katika tukio
jingine lililotokea usiku wa kuamkia leo Jumatano, mwendesha pikipiki mmoja
Kitaboka Maringo Matutu Issa, mkazi wa mjini Bunda, ameuawa na mtu au watu
wasiofahamika kwa kupigwa na kitu kizito kichwani, pamoja na kuchomwa shingoni
na kitu chenye ncha kali.
Tukio hilo ambalo
pia lilithibitishwa na polisi limetokea katika mtaa wa Manyamanyama kata ya
Nyasura mjini Bunda.
Afisa mtendaji wa
kata ya Nyasura, John Yapanda, amesema kuwa mwendesha pikipiki huyo aliuawa
kikatili na watu hao ambao pia walimpora pikipiki yake.
Kamanda wa polisi
mkoani Mara, kamishina msaidizi mwandamizi wa polisi, Ferdinand Mtui, leo
hakupatikana kuzungumzia matukio hayo, kutokana na pilikapilika za
shughuli za msiba wa mkuu wa mkoa wa Mara, John Gabriel Tupa, aliyefariki dunia
ghafla jana akiwa wilayani Tarime, alikokuwa amekwenda kufunga mafunzo ya
mgambo.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment