MAC PRODUCTION STUDIO'S

MAC PRODUCTION STUDIO'S
KWA MATANGAZO YA BIASHARA REDIONI( 0767-814844)

Monday, 5 May 2014

NEWS ALERT!!!SERIKALI KUENDESHA SHUGHULI ZAKE KWA UWAZI

Serikali imesisitiza nia yake ya kuendesha shughuli zake kwa uwazi na kusema maandalizi ya kutunga sheria ya haki ya kupata taarifa kutoka kwa taasisi za umma yameanza kuongeza uwazi katika uendeshaji wa shughuli za serikali.
Waziri wa Katiba na Sheria Dr. Asha-Rose Migiro akiwasilisha taarifa ya makadirio ya bajeti ya Wizara yake kwa Kamati ya Bunge ya Katiba


Akiwasilisha taarifa ya makadirio ya matumizi kwa mwaka ujao wa fedha kwenye Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala jijini Dar es Salaam jana (Jumamosi, Mei 3, 2014), Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro alisema dhamira hiyo inatokana na matakwa ya Katiba kuhusu haki ya kupata taarifa, Mpango wa Kimataifa wa Uendeshaji wa Serikali kwa Uwazi (OGP) na ahadi ya Rais Kikwete.

“Azma ya Serikali ni kuendesha shughuli zake kwa uwazi zaidi katika Nyanja mbalimbali za huduma…hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba sambamba na Mpango wa Kimataifa wa Uendeshaji wa Serikali kwa Uwazi (OGP),” alisema Waziri Migiro na kuongeza:

“Wizara imeandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu kutunga sheria ya Haki ya Kupata Taarifa kutoka taasisi za umma na ni matarajio ya Wizara kuwa mchakato huu utakamilika kabla ya mwezi Disemba, 2014,” alisema katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki na viongozi wengine wa Wizara na taasisi zake.

Katika mkutano huo, Waziri Migiro pia alizungumzia mpango wa Wizara yake wa kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani ambapo Mahakama ya Tanzania imeanzisha mpango wa ufanyaji kazi kwa kujipima.

Kwa mujibu wa Dkt. Migiro, utaratibu huo unaweka wastani wa idadi ya mashauri yatakayotolewa uamuzi na Majaji na Mahakimu katika kila ngazi ya Mahakama kwa kila mwaka.

“Katika Mahakama ya Rufani lengo ni kumaliza wastani wa mashauri 1,200 hadi 1,400 kwa mwaka, Mahakama Kuu mashauri 200 hadi 250 kwa kila Jaji kwa mwaka , na Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya mashauri 250 hadi 300 kwa kila Hakimu kwa mwaka,” alisema Waziri Migiro katika mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Waziri Migiro, ambaye aliteuliwa na Rais Kikwete kuongoza Wizara hiyo mapema mwaka huu, alifafanua kuwa utaratibu huo umeshaanza kufanya kazi na umeonyesha mafanikio makubwa.

Pamoja na utaratibu huo, Waziri Migiro pia alizungumzia jitihada za Serikali za kupunguza mlundikano wa wafungwa na mahabusu magerezani kupitia mpango maalum wa kutenganisha shughuli za mashtaka na upelelezi.

Kwa mujibu wa Waziri Migiro, kupitia mpango huu, Mkurugenzi wa Mashataka huchuja majalada yanayowasilishwa kwake na taasisi za upelelezi kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa.

“Mkurugenzi wa mashtaka ndiye mwenye mamlaka ya kutoa hati ya mashtaka baada ya kujiridhisha na ushahidi unaowasilishwa na vyombo vya upelelezi, hivyo kupunguza kwa mlundikano wa mashauri mahakamani kutokana na utaratibu huu wa kuchuja majalada,” alisema 

Na Mwanaharakati.

No comments: