Mganga wa asili anayemtibu Luhogola |
Aliyezimia baada ya kuona uozo wa makalio |
Aliyetimuliwa Hospitalini hapo ni
Joseph Luhogola (38),mkazi wa Kitongoji cha Nyabugera,Kijiji cha Mganza Wilaya
ya Chato katika Mkoa wa Geita.
Luhogola alipokelewa Hospitalini
hapo Apr 22 mwaka huu akitokea katika Hospitali ya Wilaya ya Chato ikiwa ni saa
chache baada ya kupata ajali.
Ajali hiyo ilitokea Apr 22 katika
Kijiji cha Lubambagwe Wilayani Chato,ambapo gari aliyokuwa ameipanda Luhogola
aina ya Hiace akitokea Geita kwenda Mganza ilipofika eneo hilo na kupinduka
baada ya kuchomoka gurudumu la mbele na baadaye la nyuma.
Kufuatia ajali hiyo iliyotokea
majira ya saa 7 mchana,Luhogola huku akiwa amepoteza fahamu alikimbizwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Chato ambako hata hivyo alipatiwa huduma ya kwanza kabla
ya kuchukuliwa na gari la Hospitali hiyo hadi Bugando.
Kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando
alipokelewa na kulazwa wodi E namba 803 ambayo ni ya wanaume iliyoko
katika ghorofa la 8 kwenye majengo ya Hospitali hiyo.
Hata hivyo imeelezwa kuwa,baada ya
madaktari kuchunguza afya yake ilibainika kuwa alikuwa na tatizo la uti wa
mgongo na alishauriwa kulala chali muda wote kama tiba ya tatizo alilokuwa
nalo.
Wakati wote akiwa Wodini hapo,mke
wake Keflini Kafaransa(36) alikuwa akizuiwa kukaa wodini kwa
mumewe kwa alichoelezwa sheria za Hospitali hiyo haziruhusu mwanamke
kukaa kwenye wodi ya wanaume kwa muda mrefu.
Kutokana na hali hiyo,Kafaransa
alilazimika kumtafuta shemeji yake Hatari Petro(21)ambaye ni mdogo wa Luhogola
na ndiye aliyechukua jukumu la kumuuguza kaka yake huyo kuanzia Apr 28 hadi
anatimliwa kwenye hospitali hiyo.
Akisimulia mkasa huo,Luhogola ambaye
kwa sasa yu mahututi nyumbani kwa mganga wa tiba za asili za mifupa katika
Kitongoji cha Elimu,Kijiji cha Nyankumbu Wilayani Geita alisema hakutegemea
kama Hospitali kubwa kama Bugando ingeweza kumuaga akiwa katika hali hiyo.
Luhogola ambaye kwa sasa amepooza
kuanzia kifuani hadi miguuni anadai kuwa,iwapo angejua hayo yangetokea
angewashauri ndugu zake wasimpeleke kwenye Hospitali hiyo kwa kuwa tatizo
alilonalo la kuoza makalio yake lilisababishwa na wauguzi waliokuwa
wakimhudumia.
CHANZO CHA AJALI YAKE
Akifafanua ajali
ilivyotokea,Luhogola alisema ‘’Nakumbuka nilikuwa mbele kwa dereva ,gari
ilibasti tairi ya nyuma na baadaye ya mbele ilikuwa mwendo kasi na kuhama
barabarani,gar iliviringika na mimi nikiwa mbele nilipitia kioo cha mbele cha
dereva nilikuwa natoka Geita na sikujua tena kilichoendelea hapo maana
nilipoteza fahamu na nilipoijiwa na fahamu nilikuwa Bugando na nikagundua
nimeumia kichwani na kifuani’’
AKIWA BUGANDO
‘’Nakumbuka nilipopata fahamu nikiwa
Bugando,niligundua nina majeraha madogo madogo sehemu za kichwani ambayo hata
hivyo hayakuchukua muda na yalipona kwa muda mfupi lakini niliendelea kukaa
wodini hapo baada ya madaktari kunieleza ninatatizo la uti wa mgongo’’
‘’Nilipowauliza tiba za
ugonjwa huo daktari aliyekuwa anakuja kunitizama wodini hapo alinieleza
kuwa,hakuna tiba ya ugonjwa huo zaidi ya kulala chali bila kugeuzwa
geuzwa name nikakubali’’
‘’Hata hivyo nikiwa wodini hapo
nilipooza mwili kuanzia kifuani hadi miguuni hivyo nikapoteza mawasiliano
kutoka sehemu ya mwili ulioopooza hadi miguuni’’
Alidai kuwa,kutokana na kupooza
kwake hakuweza kujua kinachoendelea na alikuwa akiona manesi wakimfuata
alipolala kisha kumgeuza kifudifudi na baadaye kumlaza chali kama maelekezo ya
daktari aliyedai hiyo ndiyo tiba ya uti wa mgongo.
Alidai kuwa,siku moja baada ya
manesi kumlaza kifudifudi kwa muda mrefu na baadaye kumlaza tena chali aliamua
kuhoji na ndipo alipoelezwa anakijiupele kidogo sehemu za makalio‘’
‘’Ilikuwa kama ada ya manesi kufika
na kunigeuza nalalia tumbo(kifudifudi)bila kujua walichokuwa wanakifanya maana
kutokana na kupooza kwangu sikuhisi maumivu yoyote’’
‘’Hata hivyo mtindo huo uliendelea
siku baada ya siku na ndipo siku moja nilipoamua kuhoji kulikoni baada ya
kunilaza kifudifudi kwa muda mrefu na ndipo waliponiambia nina upele kwenye
makalio hivyo walikuwa wananisafisha’’alisema Luhogola kwa sauti isiyo na
matumaini.
Kutokana na majibu hayo ya
manesi,Luhogola alidai kuwa manesi hao waliendelea na utaratibu huo hadi
alipoagwa Hospitalini hapo akiambiwa amepata nafuu bila kujua makalio yake
yalikwisha oza hadi kwenye uti wa mgongo huku ndani ya kidonda kukijazwa
bandeji kumwezesha kukaa.
‘’Mimi nahisi Madaktari walikuwa
hawajui kama nakidonda na manesi ndio waliwaficha madaktari,maana manesi
walikuwa wananigeuza na kunisafisha na kunirudisha hivyohivyo’’
‘’Nikiwauliza manesi mbona
wananisafisha muda murefu wanadai hakuna kitu maana sina hisia za maumivu
yoyote’’alisema kwa sauti ya kukwaruza
MKEWE AZUNGUMZA
Akizungumza na JAMHURI mke wa
Luhogola,Kefline Kafaransa(36)alidai kuwa muda wote waliokuwa wodini hapo
hakuweza kubaini janja nyani ya manesi waliokuwa wakimhudumia mumewe ya kujaza
bandeji sehemu ya makalio kilipo kidonda hicho.
Kafaransa anataja sababu za
kutogundua iwapo mumewe alikuwa na kidonda kikubwa kwenye makalio ambacho
kilijazwa mabandeji na manesi hao kwa kuwa muda wote alipokuwa akiingia wodini
hapo alifukuzwa na wauguzi hao.
‘’Yaani ile wodi nilipokuwa naingia
kumjulia khali mume wangu,manesi walinifukuza hivyo sikuweza hata kubaini kama
mume wangu anakidonda kikubwa kiasi kile na siku zote niliambiwa ile ni wodi ya
wanaume mimi kama mwanamke sipaswi kukaa mle kwa muda mrefu’’
Kufuatia hali hiyo Kafaransa anadai
kuwa,hakuona huduma yoyote aliyokuwa akifanyiwa mumewe huyo zaidi ya kumkuta
akiwa amelala chali muda wote.
Kwa mjibu wa Kafaransa,mbali na
madaktari kumweleza mumewe angelikaa wodini hapo kwa muda wa wiki 6 akipatiwa
huduma ya tiba za uti wa mgongo alishangaa kuona wakiagwa Mei 27 kabla ya muda
huo huku wakitozwa gharama kubwa tofauti na huduma yenyewe.
‘’Madaktari baada ya kutupokea na
kugundua tatizo la mume wangu walidai kuwa tiba ya mtu mwenye tatizo hilo
lazima akae wodini kwa muda wa wiki 6 lakini nilishangaa kuona tunaagwa kabla
ya muda huo huku gharama tulizotozwa zikiwa ni kubwa.
‘’Wakati tulikwishaambiwa tutakaa
pale na mgonjwa wetu kwa wiki 6,nilishangaa Tarehe 26 baada ya daktari kupita
mzunguko 27/05/2014 saa 6 tuliagwa rasmi kwa kulipa madeni yote
tuliyokuwa tunadaiwa kiasi cha Tshs 119,000.00 kama malipo ya huduma
tuliyoipata hospitalini hapo pesa ambayo ni kubwa na nadhani tulitozwa ili
kununua kidonda alichokipata akiwa wodini hapo.
MDOGO WAKE ANENA
Kwa upande wake,Hatari Peter(21)ambaye
ndiye alikuwa akiingia wodini hapo mara kwa mara kumjulia hali kaka yake huyo
alidai kuwa hata yeye hakuweza kubaini iwapo kaka yake ameoza sehemu za makalio
kwa kile alichodai muda wote alimkuta amefunikwa shuka la Hospitali hiyo.
Peter ambaye alikuwepo wodini hapo
wakati wakiagwa,alidai kuwa huku akijua kaka yake amepata nafuu kwa mjibu wa
daktari aliyemuaga,walielezwa kuwa watafute gari ya kukodi ili wamlaze kaka
yake juu ya godoro hadi nyumbani.
Daktari aliyewaaga aliwaambia hata
wakifika nyumbani waendelee kumlaza chali mgonjwa wao hadi hapo mgongo
utakapotengemaa vizuri huku wakionywa kutomfanyisha kazi ngumu.
‘’Yaani yale maneno matamu aliyokuwa
akitueleza Yule daktari kwa mtu yeyote angehisi kuwa mgonjwa wetu ameshapona
kabisa kumbe walikuwa wametuingiza mjini kwani kama tungejua kaka hana makalio
na anakalia bandeji tusingekubali kumtoa hapo wodini na kama noma basi ingekuwa
noma’’alisema na kuongeza
‘’Yule daktari kwa kinywa chake
alitutamkia kwamba hali ya kaka kwa muda huo ilikuwa imetengemaa kabisa tena
akamwambia na kaka kwa kumhusia ‘’Joseph uende nyumbani ,wakukodishie Gari
wakubebe waweke godoro na ukifika nyumbani uendelee kulala mpaka mwezi wa nane
‘’alisema Peter akinukuu maneno ya Yule Daktari na kuongeza
‘’Akamuuliza tena kaka ‘’Joseph
unafanya kazi gani,alipojibiwa ni mfanyabiashara wa dagaa daktari Yule
aliongeza ‘’Hiyo biashara huiwezi na kama ndugu yako ana uwezo wakununulie
baiskeli ya miguu mitatu na wakufungulie biashara ya kibanda uwe unauza sawa
Joseph”alisikika akimhusia mgonjwa wao baada ya kuagwa hospitalini hapo.
Kwa mjibu wa Peter,walifanya kama
walivyoelekezwa kwa kukodi gari kisha kumlaza kwenye godoro hadi nyumbani kwa
kaka yaom aishie mjini Geita ambako ndiko walipogundua kuwa makalio yake
yameoza huku kukiwa kumejazwa bandeji ndani yake.
ALIYEMPOKEA APOTEZA FAHAMU BAADA YA
KUGUNDUA KIDONDA
Msitapher Luhogola(40)ambaye ni kaka
wa mgonjwa huyo aliyepooza na kukosa matumaini huku akitibiwa kwa tiba za jadi
anadai kuwa yeye ndiye aliyegundua kidonda hicho muda mfupi baada ya kumpokea
akitokea Bugando hali iliyopelekea kupoteza fahamu kutokana na mshituko
alioupata baada ya kuona kidonda hicho.
Msitapher alifafanua kuwa,baada ya
kumpokea mdogo wake huyo,ambaye alikuwa amevalia nguo zake nzuri aligundua
harufu Fulani wakati akimshusha kwenye gari iliyomtoa Bugando akimuingiza ndani
ya nyumba yake na kuamua kuchunguza kwa makini harufu ilikokuwa ikitokea kwenye
mwili wa ndugu yake huyo.
‘’Baada ya kumfikisha nyumbani ndio
niligundua anatoa harafu ikabidi nimlaze kitandani na kuanza kumkagua na ndipo
nikagundua alikuwa amezungushiwa bandeji sehemu ya makalio yake nikachukua
jukumu la kumfungua bandeji zile ili kuona na ikibidi nimsafishe’’
‘’Ndugu yangu,nilijikuta napiga
kelele kama mtu aliyeona mnyama mkali kwani sikuamini kama ningekuta ndugu
yangu hana makalio yalishaoza maana nilikuta kwenye makalio amerundikiwa
mabandeji lundo yamesondekwa kilipo kidonda’’.
Msitapher (36) ambaye alimpokea ndugu
yake huyo majira ya jioni ya Mei 27 anadai kuwa, baada ya
kufungua kisha kutoa yale mabandeji yaliyokuwa yamesondekwa ndani ya
kidonda hicho alijikuta akipoteza fahamu na kuwalazimu ndugu na jamaa waliokuwa
wamekusanyika chumbani humo kufuatia kelele alizopiga kuanza kumpepea na
alizinduka baadaye huku asijue la kufanya.
‘’Baada ya kurejewa na fahamu ndiyo
nikaanza kukiosha na mpaka sasa naendelea kukiosha na tupo kwa mganga huyu wa
jadi ambaye anamtibu kwa tiba za kienyeji kwa maana dawa za kizungu
zimeshindikana’’
‘’Kama wamemfukuza hospitali,sisi
kama ndugu tumetafuta mbadala mwingine kuhakikisha tunaokoa maisha ya
mwenzetu’’alisema kwa uchungu na kuongeza
‘’Sikuamini kama hospitali kama
Bugando ambayo ni ya rufaa kama inaweza kufikia hatua ya mgonjwa kuoza wakati
kuna wataalamu wa kutosha na wakamuaga mtu mwenye kidonda kama hicho,kwa hiyo
orodha ya pesa tuliyolipa tulikuwa tunanunua kidonda ambacho kimesababishwa na
hospitali hiyo’’
‘’Au tunachangia hiyo pesa jengo la
Bugando liendelee kuwepo kama Bugando au pesa hiyo ni kwa manufaa ya madaktari
na wauguzi mpaka sasa sielewi,kama kuna msaada zaidi juu ya matibabu
hasa kama haya ambayo wamesababisha wenyewe kwa mgonjwa basi Serikali iingilie
kati hasa waziri wa afya ili ndugu yangu asaidiwe’’alisema kwa masikitiko.
NYARAKA ZA HOSPITALINI HAPO
Jamhuri limebahatika kuona nyaraka
mbalimbali ambazo zinadhihirisha kwamba,mgonjwa huyo amewahi kulazwa katika
hospitali hiyo kabla ya kuagwa.
Nyaraka hizo pamoja na mambo mengine
zinaonyesha kiasi cha pesa walizolipa Hospitalini hapo,baadhi ya madaktari na
wauguzi waliompokea na kumhudumia,na namba 973807 ambayo ndiyo ulikuwa usajili
wa mgonjwa huyo kuingilia kwenye Hospitali hiyo.
Baadhi yao ni Dokta Ernest Etuonguo
aliyempokea Apr 22,Dokta G. Daniel aliyechunguza afya yake,pamoja na Dokta
Shanel aliyemuaga Mei 27,huku muuguzi aliyefahamika kwa jina la Mage akidaiwa
ndiye aliyekuwa wodini hapo akitoa huduma mbalimbali ikikwemo dawa kwa mgonjwa.
MTOA TIBA ZA JADI ATOA YA MOYONI
Kwa upande wake Paul Chasama ambaye
ni mtaalamu wa tiba za jadi kwa kuunga mifupa na kurudisha viungo
vya mwili vilivyochengana ambaye ni mkazi wa Kitongoji cha Elimu,katika kijiji
cha Nyankumbu Wilayani Geita amedai kuwa,kutokana na uzoefu kwenye kazi hiyo
anao uhakika wa asilimia mia kwamba Luhogola atapona.
Chasama aliyedai kurithishwa ujuzi
huo na marehemu baba yake mzee Chasama Luswigilo alidai kuwa,kutokana na uzoefu
wake wa miaka mingi kwenye kazi hiyo ndugu wa mgonjwa waendelee kumwamini kama
walivyomwamini kumkabidhi mgonjwa wao na kwamba si muda mrefu atarejea katika
hali yake ya kawaida.
Akifafanua kauli yake,Chasama alidai
kuwa,amekwishakutana na wagonjwa wengi wenye matatizo makubwa
tofauti na alilonalo Luhogola na walipona na kurejea katika afya zao na kwamba
kwa uzoefu wake katika kipindi cha mwezi mmoja mbele atakuwa amepona.
‘’Mimi ndiye Chasama kama umewahi
kumsikia ninachokueleza ndugu mwandishi huyu mgonjwa katika kipindi cha mwezi
mmoja mbele atakuwa anadunda mtaani kwa hili tatizo la kupooza kwake,na
kuvunjika uti wa mgongo na hata hiki kidonda ndani ya wiki tatu kitakuwa
kimepona maana nimeshaanza kuweka dawa ya kuotesha nyama’’alitamba Chasama
Akielezea chanzo cha wagonjwa wa
kupooza,alidai kuwa hutokana na mshituko ambao husababisha mipira iliyo ndani
ya mgongo kukatika na kupoteza mawasilianao ya mwili.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya
Bugando iliyopo Jijiji Mwanza Profesa Charles Majinge alipotafutwa kwa njia ya
simu yake ya kiganjani namba 0754-454724 ili kuzungumzia sakata hilo
hakupatikana na hata alipopatikana simu yake ilionyesha imepokelewa na baadaye
ilizima.
Jamhuri halikuchoka liliamua
kumwandikia ujumbe wa maandishi kuuliza iwapo wataalamu wa hospitali hiyo
walishindwa kutibu kidonda hicho na badala yake kuamua kukificha kwa kukijaza
bandeji hadi kilipogunduliwa na ndugu zake baada ya kufikishwa nyumbani kwako, hata
hivyo hakujibu. Hata hivyo Jamhuri litaendelea kumtafuta na litawajuza wasomaji
wake hatua kwa hatua juu ya sakata hili.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment