Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema
kuwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ni mzuri, umeleta matumaini kwa kupanua
wigo na kufungua zaidi uwanja wa kisiasa pamoja na kuiwajibisha Serikali.
Hata
hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa ili mfumo huo uboreshwe zaidi na uweze
kuimarisha misingi mikuu ya maendeleo ni lazima uendeshwe kwa watu kufuata
sheria na wala siyo kuingiza matumizi ya nguvu ambayo yanaweza kuvuruga nchi.
Rais
Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama
aliyasema hayo jana Ijumaa, Juni 20, 2014, wakati alipotoa Mhadhara (Lecture)
kuhusu Usalama wa taifa – The Security of a Nation- kwenye Chuo cha Taifa cha
Ulinzi - National Defence College (NDC)
Kunduchi, mjini Dar es Salaam.
Rais
Kikwete alikuwa anajibu swali la mwanafunzi wa kozi ya pili kwenye chuo hicho
kutoka Kenya ambaye alitaka kujua jinsi gani vyama vingi vya siasa
vinavyoathiri umoja wa kitaifa na kuibadilishaTanzania kufuatia miaka zaidi ya
30 ya Tanzania kuwa nchi yenye kuleta matumaini kwa nchi nyingine za Afrika na Waafrika.
Rais
kikwete alisema: “Vyama vingi ni vizuri. Mfumo wa vyama vingi unaleta matumaini
kwa kupanua wigo wa kisiasa ambao haukuwa mpana kiasi hicho huko nyuma. Sasa
mtu anaweza kuamua kujiunga na chama chochote cha siasa anachokipenda yeye.”
Aliongeza
rais Kikwete: “Ni mfumo ambao unaiwajibisha Serikali. Ni mfumo mzuri kwa
upanuzi wa demokrasia. Sasa watu wanaweza hata kuamua kupunguza bajeti ya
safari za Rais nje ya nchi. Wanadhani kuwa Rais anaweza kufanikiwa zaidi na
Tanzania kupita hatua za maendeleo haraka zaidi kama Rais atabakia amejifungia
ndani ya nchi.”
Rais
Kikwete alizidi kujibu swali hilo: “Jambo la maana ni kwamba tunahitaji aina
mbali mbali za mawazo. Mawazo ya namna hiyo hayaathiri demokrasia. Mawazo ya
namna hiyo yanasaidia hata chama changu kuimarika zaidi.”
Hata
hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa mfumo huo utavurugika endapo baadhi ya watu
wataendekeza matumizi ya nguvu na hoja za nguvu badala ya kupambana kwa hoja na
nguvu ya hoja.
“Wasiwasi
wangu ni kuingiza matumizi ya nguvu katika ujenzi wa demokrasia. Ni makosa kwa
watu kukimbilia kutumia nguvu baada ya kushindwa kwenye hoja. Na hili
halivumiliki na likitokea basi Serikali itaingilia kati kudumisha amani.”
Imetolewa
na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
21 Juni,2014
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment