![]() |
Wimbo wa mdogomdogo waendelea kuongoza kusikilizwa kwa wiki ya kumi katika Marimba music chart |
Hii ni mara ya pili kwa Diamond
kusababisha vurugu nchi za ughaibuni baada ya Septemba 1, kusababisha vurugu
katika mji wa Stuttgart nchini Ujerumani aliposhindwa kufika kwa wakati
ukumbini.
Akizungumza na mwandishi, shuhuda wa
tukio ambaye ni Mtanzania anayefanya shughuli zake nchini Uingereza, Flora Lyimo
alionyesha wazi kukerwa na tukio hilo ambalo alieleza kuwa huenda likaharibu
sifa ya nyota huyo ughaibuni.
Lyimo ambaye alihudhuria shoo hiyo
alisema Diamond alisubiriwa na zaidi ya watu 200 tangu saa sita usiku bila
nyota huyo kutokea na ilipofika saa 10:00 alfajiri, ndipo walipoanzisha vurugu
kudai kurudishiwa pesa zao.
Shoo hiyo ambayo ilitozwa kiingilio
cha pauni 20 sawa na fedha za Tanzania Sh54,280 iliishia kwa dosari ya aina
yake baada ya polisi kulazimika kuingilia kati kusimamia urudishwaji wa fedha
hizo.
Alisema waliamuru watu warudishiwe
fedha zao, hivyo walipanga mstari na kurudishiwa fedha zao, kila mmoja
akiamuriwa kuondoka eneo hilo huku wenye klabu hiyo wakinyang’anywa leseni.
“Ni jambo
la ajabu na aibu kwa msanii ambaye Watanzania tunamtegemea atuwakilishe nje ya
nchi anakubali vipi kutangazwa kwenye shoo kama hajalipwa pesa zake, watu
wanamchukulia kama tapeli kwani yeye mwenyewe amewatangazia mashabiki wake
halafu hajatokea.
“Wengi
tunapata shaka kama hajashirikiana na huyo promota kwani hata huo ukumbi ambao
shoo ilitakiwa kufanyika hauna jukwaa maalumu ambalo msanii anaweza kutumbuiza
binafsi nilishangaa haikuwa eneo sahihi, lakini nikasema ngoja niende kumuunga
mkono Mtanzania mwenzangu,”alisema
Lyimo.
Hata hivyo, pesa zilizopatikana
hazikutosha kuwarudishia watu wote ikizingatiwa kuwa wengi walikata tiketi
kabla ya siku ya shoo, hapo ndipo vurugu zilipotokea na polisi kulazimika
kumshikilia promota wa shoo hiyo ambaye alifahamika kwa jina la Victor.
“Polisi
wengi sana waliofika hapa ukumbini kwa ajili ya kulinda usalama, walichokifanya
ni kumchukua promota aliyeandaa shoo hii na kumweka chini ya ulinzi kwa kosa la
utapeli, kwa sharti kwamba mpaka watakapompata Diamond, lakini mpaka sasa bado
haijajulikana alipo,” alisema Lyimo.
Lyimo alionyesha wasiwasi wake na
kueleza kuwa kutokana na mfululizo wa matukio hayo huenda Diamond akazuiliwa
kufanya shoo katika nchi za Ulaya, kutokana na kuanza kupoteza imani kwa
mashabiki wake.
Mwandishi alimtafuta balozi wa Tanzania nchini Uingereza,
Peter Kallaghe ambaye alieleza kwamba hafahamu chochote kuhusu tukio hilo na
kuahidi kulifuatilia kujua undani wake.
“Kama
unasema tukio hilo limetokea usiku mimi sijapata taarifa zozote mpaka sasa,
lakini ngoja nijaribu kuwasiliana na mtu ambaye anaweza kufahamu chochote,”alisema Balozi Kallaghe.
Kwa msaada wa Balozi Kallaghe
Mwandishi alifanikiwa kuzungumza na Ofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini
Uingereza, Rahma Pompy ambaye pia alikuwa kwenye tukio hilo na kufafanua kuwa
kasoro hiyo imetokana na uzembe wa promota.
Alisema mwandaaji wa shoo hiyo
alitakiwa kumalizana na Diamond kabla ya kuwajaza watu ukumbini, lakini
hakufanya hivyo hali iliyosababisha nyota huyo kushindwa kufanya kilichompeleka
na kufafanua kuwa hii siyo mara ya kwanza kwa promota huyo mwenye asili ya
Tanzania kufanya uzembe wa aina hiyo.
“Kwa mimi
niliyekuwepo eneo la tukio nafahamu fika kuwa Diamond hakuwa na kosa lolote,
hakulipwa na wala promota hakumfuata hotelini. Unafikiri angeweza vipi kufanya
kazi ya namna hiyo,” alisema.
Ingawa mashabiki wengi hawakumwona,
lakini Pompy alibainisha kuwa Diamond alifika eneo hilo saa tisa usiku, hata
hivyo alishindwa kuingia ndani ya ukumbi huo kutokana na kutomalizana na
promota.
“Watu
wengi hawakumwona ila mimi nilimwona Diamond, alifika na alionyesha wazi namna
alivyokuwa akihangaika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo ili kuwaridhisha
mashabiki wake, lakini alishindwa kwa sababu hakuwa amelipwa na muda ulikuwa
umekwisha,” alisema.
Ilikuwaje Diamond akawasili saa tisa
usiku?
Kwa mujibu wa Pompy, baada ya
Diamond kusubiri kwa muda mrefu hotelini bila kufuatwa na promota, akaamua
kwenda mwenyewe kwenye ukumbi alikotakiwa kufanya shoo. Hata hivyo, alikumbana
na usumbufu mkubwa njiani kutokana na barabara nyingi kufungwa nyakati za usiku
kutokana na matengenezo.
“Kuna
matengenezo ya barabara nyingi zinafungwa, hivyo akajikuta anazunguka kwa muda
mrefu kutafuta njia mbadala. Mpaka alivyofika ukumbini, ilikuwa tayari
imeshafika saa tisa, hata hivyo asingeweza kufanya chochote kwa kuwa
hakumalizana na promota na ukumbi aliotakiwa kufanya shoo unafungwa saa 9:30,
nadhani hata yeye alikuwa hafahamu,” alifafanua.
Kuhusu taarifa za Diamond kutafutwa
na polisi kutokana na tukio hilo, Pompy alisema hana uhakika na uvumi huo kwa
kuwa makosa yalionekana wazi kuwa ni ya promota.
Meneja wa Diamond afunguka
Kutokana na tukio hilo, Meneja wa mwanamuziki huyo, Hamis
Taletale maarufu Babu Tale ambaye hakuambatana naye, amesema kuwa Diamond
alipokea mwaliko kutoka kwa promota huyo, lakini hakulipwa fedha hata kidogo,
jambo ambalo lilimfanya ashindwe kufanya uamuzi wowote.
“Diamond
alipofika Uingereza yule promota alimdaka juu kwa juu kwa kuwa kule alikwenda
kwa ajili ya shoo ya Ujerumani itakayofanyika usiku wa leo (jana) akimtaka
afanye shoo jijini London, Uingereza, alikubali na baada ya hapo alisema kuwa
angemlipa siku ya shoo, lakini kwa wakati wote hakufanikiwa kuonana naye tena,
alikuwa akiwasiliana naye kwa simu tu,”
anaeleza Taletale.
Alisema Diamond alimsubiri promota
huyo kwa muda mrefu, licha ya kufanya matangazo aliamini kuwa kabla muda wa
shoo haujafika angemlipa fedha ili aende ukumbini.
“Diamond
alishangaa kuona ilipofika saa nne usiku wa kuamkia jana promota yule
hapatikani, kwa kuwa hakulipwa hata dola moja (Sh1,600) aliamua kutulia
hotelini kwani promota ndiye anatakiwa amfuate msanii, na yeye hakufanya hivyo
wala hakumlipa hata kidogo. Msanii wangu hana makosa ndiyo sheria ya kazi
ilivyo,” alisema Taletale.
Hata hivyo, Taletale alisema
wamiliki wa ukumbi ndio walioamua kuita polisi baada ya kuona viashiria vya
vurugu, na hapo ndipo ilipogundulika kuwa promota huyo hakulipia ukumbi pia.
“Licha ya
kwamba hakumlipa msanii wangu, pia ukumbi hakuulipia. Alichokifanya mmiliki ni
kurudisha fedha kwa watu waliohudhuria mbele ya polisi na promota yule
akakamatwa.”
Akizungumzia usalama wa Diamond,
Taletale alisema, “Msanii wangu yupo
katika mikono salama na hivi tunavyoongea ameshapanda ndege kuelekea Ujerumani
kwa ajili ya shoo jioni ya leo. Hana kosa lolote, hakuna mkataba baina yake na
promota unaoonyesha kwamba alilipwa,hivyo hakuwa na kizuizi na polisi
hawajashughulika naye,” alisema Taletale.
Hata hivyo, alipoulizwa kwa nini
anamwacha msanii wake asafiri peke yake na kufanya makubaliano na mapromota
kazi ambayo alitakiwa aifanye yeye (Taletale) alisema:
“Ilikuwa
nisafiri naye, lakini kwa bahati mbaya kulikuwa na matatizo ya kifamilia ambayo
ilinilazimu nibaki nchini. Yeye alikwenda kwa ajili ya shoo mbili zilizofanyika
Jumamosi Afronation na hii ya leo itakayofanyika Sturtgart. Huyu promota
alimdaka tu,” alisema Babu Tale.
Baada ya kutokea kwa vurugu hizo,
mwanamuziki Diamond alisema promota huyo amemtapeli kwa kuwa hayakuwa makubaliano
yao awali.
“Tafadhali
ndugu zangu wa Uingereza haikuwa dhamira yangu, kuweni makini sana na promota
huyu Victor Dj Rule, mnaposikia kaandaa shoo, pati au hafla yoyote ni vyema
kuziepuka na kutohudhuria kabisa kwa sababu ni tapeli, si unajua aisifiaye mvua
imemnyeshea, basi miye nimeloa kabisa,”
aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Akizungumzia sakata hilo, Rais wa
Shirikisho la Muziki Tanzania, Ado Novemba alisema tatizo alilopata Diamond
limepokewa kwa masikitiko makubwa na wanamuziki wote nchini.
“Tunasikitika
kwani hii ni mara ya pili inatokea tena kwa kipindi cha mwezi mmoja, lakini
baada ya kufanya mawasiliano, tumegundua tatizo lilikuwa la promota,
mwanamuziki wetu hana hatia na ameshaondoka Uingereza leo (jana) asubuhi na sasa
yupo Ujerumani kwa ajili ya shoo nyingine ya usiku wa leo,” alisema Ado.Na Mwananchi.
No comments:
Post a Comment