Tanzania
inatarajiwa kupata sheria ya Uhuru wa kupata Habari ifikapo Mwezi Februari, Mwaka
2015.
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo jana tarehe 24 Septemba, 2014 jijini New
York alipokuwa mmoja wa wazungumzaji katika mkutano unaohusu Uwazi na
ushirikiano kati ya serikali na jamii (Open Government Partnership-OGP).
Rais
Kikwete amesema, rasimu ya muswaada wa Uhuru wa kupata Habari uko katika hatua
ya mwisho ambapo wadau mbalimbali wanashauriana na kutoa maoni tayari
kupelekwa bungeni.
"Muswaada
huo unatarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza Mwezi Novemba mwaka huu, na kufikia
Mwezi Februari mwakani sheria mpya ya kupata Habari itakua tayari"
amesema.
Mwezi
Oktoba Mwaka 2013 katika mkutano wa OGP jijini London, Rais Kikwete alitangaza
nia na ujasiri ulioko Serikalini kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na sheria ya
Uhuru wa Habari.
Rais
amesema, Uhuru wa Habari ni muhimu kwa wananchi kwa sababu "Ni haki yao ya
msingi na kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi yanayofaa kuhusu maisha
yao" na kuongeza kuwa "Ni muhimu wananchi kujua serikali yao
inafanya nini kwa niaba yao" amesisitiza.
Akizungumza
katika mkutano huo, Rais Barack Obama wa Marekani amesema OGP ni ubia kati ya
Serikali na Wananchi wake. "Hakuna nchi yenye
majibu
yote kwa suala hili la Uwazi katika Serikali, tunahitaji kujifunza kutoka kwa
kila mmoja" na kuongeza kuwa ni jambo jema kwa serikali kuimarisha ushirikiano
na taasisi za kijamii.
Viongozi
wengine waliochangia katika mkutano huo ni pamoja na Indonesia , Afrika ya
Kusini na Ufaransa. Rais Kikwete yuko jijini New York kuhudhuria Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa (UN) ambapo pamoja na mambo mengine anahudhuria mikutano
mingine yenye maslahi kwa Tanzania.
Wakati
huo huo, Rais Kikwete amekutana na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Bwana
Gordon Brown ambaye pia ni Mjumbe Maalum wa UN kuhusu Elimu ambaye amemshukuru
na kumsifu Rais Kikwete kwa kusimamia Elimu nchini Tanzania.
"Tunataka
kukusaidia kufikia malengo ya milenia, tunajivunia mafanikio makubwa
uliyoyapata katika elimu" amesema Bw. Brown katika kikao hicho ambacho
kimehudhuriwa na wabia wa maendeleo ambao kwa pamoja wanataka kusaidia Serikali
katika kuleta maendeleo na kunyanyua zaidi kiwango cha Elimu nchini.
Wabia
hao ni pamoja na Shirika la Global Education, Shirika la Watoto Duniani
(UNICEF), Shirika la Misaada la Marekani (USAID), wawakilishi wa Serikali ya
Uingereza na Benki ya Dunia.
Wengine
ni kutoka Global Business Coalition na Dubai CARES ambao kwa pamoja wanataka
kuinua kiwango cha Elimu ya Msingi na Sekondari kwa kusaidia na kuchangia ili
kuboresha zaidi na kuinua kiwango cha elimu nchini.
Tarehe
25 Septemba, 2014, Rais Kikwete atahutubia Baraza la Umoja wa Mataifa
ambapo hotuba hiyo itaonekana moja kwa moja kupitia UN webcast.
......Mwisho......
Imetolewa
na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
New York - Marekani
25 Septemba, 2014
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment