Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumapili, Oktoba
12, 2014, ameungana na waombolezaji kutoa heshima za mwisho na kuaga
mwili wa Katibu Mkuu wa Kwanza Mwafrika wa Chama cha Mabunge ya Jumuia ya
Madola (CPA) Dkt. William Ferdinand Shija, ambaye pia alipata kuwa Waziri
Mwandamizi wa Serikali, katika shughuli iliyofanyika kwenye Viwanja vya
Karimjee, Dar es Salaam.
Rais Kikwete
amewasili kwenye Viwanja vya Karimjee kiasi cha saa 4:10 asubuhi kujiunga na
Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Mwenyekiti wa CPA-Kanda
ya Afrika Mheshimiwa Anne Makinda ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tanzania,
viongozi na wananchi kutoa heshima za mwisho.
Baada ya kuaga
mwili, Rais Kikwete ametia saini Kitabu cha Maombolezo ya Dkt. Shija ambaye
alifariki dunia Jumamosi ya wiki iliyopita, Oktoba 4, 2014 kwenye Hospitali ya
Charing Cross mjini London, Uingereza ambako alikuwa anapata matibabu ya
ugonjwa wa Saratani. Makazi yake ya kazi yalikuwa huko huko Uingereza.
Miongoni mwa
waombolezaji wengi kwenye shughuli hiyo ya leo ulikuwa ni ujumbe mzito wa CPA
ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Kanda ya Afrika, Mheshimiwa Lindiwe Maseko wa
Afrika Kusini. Pia shughuli hiyo imehudhuriwa na Bwana Joe Omoldin ambaye sasa
ni Kaimu Katibu Mkuu wa Chama hicho.
Dkt. Shija
ambaye alizaliwa katika Kijiji cha Nyalukomba, Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa
Mwanza, Aprili 28, Mwaka 1947, alipata elimu ya awali maeneo ya kwako kabla ya
kujiunga na Sekondari ya Chopra mjini Mwanza kwa elimu ya sekondari na kuhitimu
ualimu katika Chuo cha Ualimu cha Chan’gombe cha Dar es Salaam Mwaka 1968.
Baadaye, Dkt.
Shija alipata Shahada ya kwanza ya Uzamili ya Uandishi wa Habari nchini India
kabla ya kupata Shahada ya Uzamivu ya fani hiyo hiyo ya Uandishi wa Habari
katika Chuo Kikuu cha Howard cha mjini Washington, D.C., Marekani. Wakati wote
wa masomo yake alikuwa Mhadhiri wa Uandishi kwenye Chuo cha Nyegezi, Mwanza.
Dkt. Shija
aligombea na kushinda Ubunge wa Jimbo la Sengerema Mwaka 1990 na kuingia
Serikali ambako alishikilia nafasi tofauti kwa vipindi tofauti kama
Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Waziri wa Habari na Utangazaji,
Waziri wa Nishati na Madini na Waziri wa Biashara na Viwanda. Dkt. Shija pia amepata kuwa Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza.
Katika Mkutano
Mkuu wake wa 52, Desemba, Mwaka 2006 mjini Abuja, Nigeria, Dkt. Shija
alichaguliwa, baada ya mchuano mkali sana, kuwa Katibu Mkuu wa Kwanza
Mwafrika wa CPA, taasisi ambayo tokea kuanzishwa kwake Mwaka 1911 ilikuwa
haijapata kumchagua Mwafrika kuwa Mtendaji Mkuu wake.
Alichaguliwa kwa
kipindi cha pili Mwaka 2012 baada ya kumaliza kipindi chake cha kwanza cha
miaka mitano. Alikuwa anamaliza muda wake Desemba 2016.
Mpaka anaaga
dunia, Dkt. Shija alikuwa ameshikilia nafasi ya Ukatibu Mkuu wa CPA kwa
mafanikio makubwa sana kwa miezi saba na miezi tisa. Atazikwa kesho, Jumatatu,
Oktoba 13, 2014 katika kijiji cha kwao cha Nyalukomba, Sengerema, Mwanza.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment