Jamaa za marehemu Paul Magu, 35, mkewe
Lydia Wangui, 35 na watoto wao Allen Muhiu (9), Ryan Ndau (8) naTiffany Wambui
(5) walishindwa kuzuia machozi na baadhi yao kuzirai wakati wa mazishi hayo.
Kasisi James Kamura wa Kanisa la
Kiangilikana Thika, alitoa mahubiri yaliyogusa wengi huku akiitaka serikali
iwaadhibu waliowaua watoto hao na mama yao.
“Ni jambo lenye uchungu sana kwa
familia kuweza kuvumilia. Ni vigumu kuelewa kilichotendeka kwa sababu wote
wamekufa. Damu ya binadamu haifai kumwagwa kama ya mnyama,” akasema Kamura.
Magu aligongwa na basi kwenye
barabara ya Thika-Garissa nao mwili wa mkewe uliokuwa na majeraha ukapatikana
karibu na hoteli ya Paradise Lost Resort, Kiambu.
Miili ya watoto wao ilipatikana
kichakani siku chache baadaye karibu Tatu City, eneo la Ruiru.
Jumanne, miili ya familia hiyo
ilipelekwa eneo la mazishi kwa magari matatu ya kubebea maiti kisha ikapelekwa
kwenye kaburi la pamoja ambapo ilizikwa.
Waombolezaji kadha walizirai na
kuondolewa eneo la mazishi.
“Haiwezekani kwamba mauaji haya
yalitekelezwa na mtu mmoja. Kuna watu walio hai waliohusika na uhalifu huu wa
kikatili na ni lazima serikali ichukue hatua,” akasema Kasisi Kamura akiongoza
ibada ya wafu katika nyumba ya wazazi wa Magu, karibu na mji wa Thika.
Wakazi walifika kwa wingi kwa ibada
na mazishi ambayo yalihudhuriwa na viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na Mbunge
wa Juja Francis Munyua. Gavana wa Kiambu William Kabogo aliwakilishwa na
msaidizi wake Sammy Onyango.
Kukatiza ibada
Mhubiri alilazimika kukatiza ibada
mara kadha na kuomba jamaa waliolemewa na huzuni wasaidiwe.
Wazazi wa mama ya watoto hao,
Francis Ndau na Mary Muthoni na jamaa zao wa karibu kutoka Kaunti ya Nyandarua
walishindwa kusimama wakati wa kuimba kwa kulemewa na majonzi.
Kasisi aliwagusa zaidi waombolezaji
aliposimulia matukio yaliyotangulia kupatikana kwa miili ya watoto hao siku
chache baada ya wazazi wao kufa katika hali ya kutatanisha.
“Mimi binafsi niliomba watoto hao
wapatikane wakiwa hai. Lakini nililia walipopatikana wamekufa. Kwa nini mtu
afanye hivi,” akashangaa.
Kasisi Kamura alisema mauaji hayo
yalihusu imani na kuwataka polisi wachunguze kilichotendeka.
“Wakenya wana haki ya kujua
yanachofunza mashirika ya kidini na vitendo vyake na ni jukumu la serikali
kuwaondoa wahubiri wanaopotosha,” akasema.
Aliongeza kuwa wakati umefika kwa
serikali kudhibiti mashirika ya kidini kwa sababu vitendo vya baadhi yake ni
vya kutiliwa shaka.
Aliwataka wafuasi wa makanisa
wakatae baadhi ya wahubiri wanaotumia dini kujitajirisha.
No comments:
Post a Comment