Kufuatia kukamilika kwa ukarabati na upanuzi wa Uwanja
wa Ndege wa Mpanda, mkoani Katavi, Serikali imewaasa watumiaji wa uwanja huo
kutunza miundombino ya uwanja huo ili kuweza kuhudumia wakazi na wageni wapitao
uwanjani hapo kwa muda mrefu.
Wito huo
umetolewa na Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya
Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati walipofanya ziara ya kukagua
maendeleo ya miundombinu katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda, mkoani Katavi.
Bibi
Mwanri alisema kuwa serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imekamilisha
kazi ya kuufanya uwanja huo uwe wa kiwango kizuri tayari kwa kutumika kwa ndege
za binafsi na biashara, hivyo uongozi wa uwanja huo hawana budi ya kuhakikisha
miundombinu ya uwanja huo inatunzwa ipasavyo.
“Kama
munavyofahamu Serikali imekuwa ikiwekeza sana katika uendelezaji wa miundombinu
ya usafiri nchini hasa kuendelea kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga ili
kuongeza ufanisi na kuendelea na kazi ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya
ndege katika maeneo ya kimkakati, hivyo kuna haja ya kuunga mkono jitihada hizi
za Serikali,” aliasa Bibi Mwanri.
Akitoa
taarifa ya uendelezaji uwanja huo kwa msafara wa timu ya ukaguzi, Meneja wa
Uwanja wa Ndege wa Mpanda, Bw Seneti Lyatuu alisema uwanja huo umeboreshwa na
hivyo, unaweza kutumika kutua na kuruka ndege za kiwango cha kati na hata zile
ndege kubwa zinaweza kutua kwa dharura.
“Uwanja
huu umekarabatiwa na barabara ya kuruka na kutua ndege imerefushwa kwa kiwango
cha lami kutoka urefu wa mita 1,500 na upana wa mita 30 hadi kufikia urefu wa
mita 1,820 na upana wa mita 30,” alisema Bw. Lyatuu.
Kwa mujibu
wa Meneja huyo, kukamilika kwa uwanja huo kumevutia idadi ya abiria wanaoutumia
uwanja huo kutoka abiria 285 mwaka 2009 hadi 2,390 mwaka 2013/14.
Kwa mujibu
wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16),
Miundombinu ni kipaumbele cha kwanza, hasa uwekezaji mkubwa katika miundombinu
ya nishati, usafirishaji (bandari, reli, barabara na usafiri wa anga), maji
(safi, taka na ya uzalishaji) na TEHAMA.
Serikali
imeandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 -2015/16) wa kutekeleza
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Lengo kuu la Mpango huu ni kufungulia fursa za
ukuaji uchumi wa nchi ili kuweka misingi ya ukuaji mpana wa uchumi na unaolenga
watu walio masikini zaidi. Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano
unawianisha katika mfumo mmoja wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa
ili kutoa mwongozo wa utekelezaji na kuipa Serikali fursa na mfumo rasmi wa
ufuatiliaji na tathmini wa miradi ya maendeleo kitaifa.
Lengo la Dira ni kuibadili Tanzania kuwa nchi ya
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment