Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi, Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa kufuatia vifo vya Mwalimu na Wanafunzi sita
waliopoteza maisha papo hapo na wanafunzi wengine 11 kujeruhiwa wakiwa darasani,
baada ya kupigwa na radi kufuatia mvua kubwa zilizonyesha zikiambatana na radi
Mkoani Kigoma.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea katika Shule ya Msingi
Nyakasanda katika ..........
Kijiji cha Nyahenda Wilayani Kasulu katika Mkoa wa Kigoma
mwishoni mwa wiki iliyoishia tarehe 22 Februari, 2015 wakati Mwalimu na
wanafunzi hao wakiwa darasani.
“Nimeshtushwa na kusikitishwa mno na ajali ya radi iliyokatisha uhai wa Mwalimu na Wanafunzi hao, hivyo kulipotezea
Taifa nguvu kazi muhimu kwa uhai na maendeleo yake”, amesema Rais
Kikwete katika Salamu zake.
“Kufuatia tukio hilo la kusikitisha, nakutumia Salamu zangu za
Rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa kuwapoteza wanafunzi hao na Mwalimu
wao.
Kwa namna ya pekee kabisa natoa pole kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya
Msingi Nyakasanda kwa pigo kubwa alilopata la kumpoteza Mwalimu na Wanafunzi
sita kwa mara moja. Naomba yeye binafsi,
Walimu na Wanafunzi wa Shule hiyo waliobaki wawe na utulivu kufuatia
mshtuko walioupata”, ameongeza kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.
Rais Kikwete ametoa pole nyingi kwa Wazazi wa Wanafunzi na Familia
ya Mwalimu waliopoteza maisha katika tukio hilo, na amewaomba wawe na moyo wa
uvumilivu na subira wakati huu mgumu wanapoomboleza misiba hii. Amewahakikishia
kuwa yuko pamoja nao katika kipindi chote cha maombolezo, na anamuomba Mwenyezi
Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Mahala Pema Peponi Roho za
Marehemu wote, Amina.
Aidha amesema anamuomba Mola awajalie Wanafunzi
waliojeruhiwa kwenye tukio hilo wapone haraka, ili waweze kurejea tena katika
hali yao ya kawaida na kuendelea na masomo yao ili waweze kutimiza ndoto zao za
maisha.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment