WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema
kuna baadhi ya watu wamegeuza mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya kuwa wa
kisiasa badala ya kujikita kuwafahamisha wananchi mazuri yaliyomo.
Ametoa kauli hiyo mwishoni mwa
wiki wakati akiwahutubia wakazi wa Kata ya Lwangwa kwenye Halmashauri ya
Busokelo wilayani Rungwe akiwa kwenye siku ya nne ya ziara yake mkoani Mbeya
kukagua shughuli za maendeleo.
“Katiba inayopendekezwa imezingatia
maslahi ya ............
kila kundi kwenye jamii hivyo zipuuzeni kauli zinazotolewa na baadhi
ya watu kuwa Katiba hiyo haijakidhi malengo ya Kitaifa,” alisema.
Alisema mabadiliko yaliyofanywa
kwenye Katiba hiyo ni asilimia 20, huku asilimia iliyobakia ni sehemu ya
mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Jaji Warioba. Alisema ili kukabiliana
na kauli za kiupotoshaji, Serikali imeanza kusambaza nakala za Katiba
inayopendekezwa hasa kwenye mikoa ya pembezoni.
“Jumla ya nakala 300 za Katiba
Inayopendekezwa zitasambazwa kwenye kila Kata ambapo makundi yenye uwezo wa
kutoa elimu sahihi kuhusiana na Katiba inayopendekezwa yatapatiwa nakala hizo
ili kuwaelimisha wananchi,” alisema Waziri Mkuu.
Wakati huohuo, akiwa Tukuyu mjini, Waziri Mkuu alizindua ofisi za
Halmashauri hiyo baada ya jengo la zamani kupata nyufa kutokana na tetemeko la
ardhi. Pia alizindua maabara tatu kwenye shule ya sekondari ya wasichana ya
Kayuki.
Akingumza na maelfu ya wakazi
waliojitokeza kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja
wa michezo wa Tandale jana jioni, Waziri Mkuu aliwataka wakazi hao kujitokeza
kwa wingi na kujiandikisha wakazi zoezi la uboreshaji Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura litakapoanza.
Alisema ni muhimu wananchi watumie
fursa hiyo ya kujiandikisha kwa sababu kadi zinazotolewa ndiyo zitatumika
kwenye upigaji kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa pamoja na Uchaguzi Mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
“Usipojiandikisha sasa hutaweza
kupiga kura kumchagua kiongozi unayemtaka wakati huo ukifika. Hata ukiwa na
kitambulisho au barua gani hutaruhusiwa kwa sababu taarifa zako zitakuwa hazimo
kwenye daftari la wapigakura.”
“Hili zoezi limeanza sasa pale
Njombe na litafanyika nchini kote, ni vema tukijitokeza kwa wingi na
kujiandikisha wakati waandikishaji watakapokuja hapa Tukuyu,” alisema Waziri
Mkuu.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Rungwe Magharibi, Prof. Mwakyusa aliiomba
Serikali iingilie kati mradi wa maji wa masoko kutokana na mradi huo kukwama
kwa muda mrefu.
“Mradi huu umelenga kuwanufaisha
wanachi wa vijiji 15, mkataba ulisainiwa tangu 2009 na mradi ulipaswa
kukamilika mwaka 2011 lakini hadi leo hakuna hata tone la maji,” alisema Prof.
Mwakyusa.
Aliiomba Serikali pia iingalie
barabara ya kutoka Tukuyu hadi Busokelo yenye urefu wa km. 86 kwani ni mkombozi
wa mazao mengi yanayozalishwa kwenye Halmashauri ya Busokelo. “Hii barabara ni
ahadi ya Mheshimiwa Rais kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami na imeingizwa
kwenye Ilani ya Uchaguzi. Kwa vile muda uliobakia ni mfupi, tunaomba iwekewe
japo jiwe la msingi ili Rais ajaye akumbuke kuikamilisha,” alisema.
Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara
yake mkoani Mbeya kwa kutembelea wilaya ya Chunya na kuzindua maabara, kufungua
mradi wa maji wa Mbuyuni.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment