Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewateua wakuu wawili wapya wa
mikoa kujaza nafasi zilizoachwa wazi na wakuu wa Mikoa ambao wanawania ubunge
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa iliyotolewa jana Jumatatu, Septemba
14, 2015 na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa katika
uteuzi wake, Rais Kikwete amemteua Ndugu Amos Makalla kuwa Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro na Ndugu Jordan Rugimbana kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Aidha, Rais Kikwete amewahamisha
wakuu wawili wa mikoa – Ndugu Mwantumu Bakari Mahiza aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa
Lindi kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Ndugu Saidi Magalula ambaye anakuwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akitokea Mkoa wa Tanga. Ndugu Magalula anachukua
nafasi iliyoachwa wazi na Ndugu Stella Manyanya anayewania ubunge mkoani Ruvuma
pia.
Ndugu Makalla ambaye alipata kuwa
Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Morogoro na Naibu Waziri wa Maji anachuku anafasi
iliyoachwa wazi na ndugu Leonidas Gama ambaye anawania ubunge mkoani
Ruvuma.
Ndugu Rugimbana ambaye alikuwa Mkuu
wa Wilaya ya Morogoro anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi kuchukua nafasi iliyoachwa
wazi na Ndugu Mahiza.
Uteuzi na uhamisho huo ulianza
Jumamosi, Septemba 12, mwaka huu, 2015 na wakuu wapya wa mikoa wataapishwa
kesho kutwa Jumatano, Septemba 16, 2015, Ikulu, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amemteua Profesa Muhammed Bakari Kambi kuwa Mganga Mkuu wa Serikali.
Taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu, Septemba 14, 2015 na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa uteuzi huo ulianza tokea Jumatano, Septemba 9, 2015. Kabla ya uteuzi wake, Profesa Muhammed Bakari Kambi alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Shirikishi cha Muhimbili, Dar es Salaam.
Vile vile, Rais
Kikwete amemteua Ndugu Mlingi Elisha Mkucha kuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika
la Maendeleo ya Taifa (NDC). Uteuzi huo ulianza Jumatano, Septemba 9, mwaka
huu, 2015.
Taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu,
Septemba 12, 2015 na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK) Ikulu, Dar es Salaam imesema
kuwa Ndugu Mlingi Elisha Mkucha ni mwanasheria kwa taaluma na mwajiriwa wa NDC
kwa miaka 14 iliyopita ambako ametumikia katika nafasi mbali mbali mpaka akawa
Kaimu Mtendaji Mkuu.
Ndugu Mkucha anachukua nafasi
iliyoachwa wazi na Ndugu Gideon Nassari aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.
Wakati huo huo, Rais
Kikwete amemteua Dkt. Tulia Ackson kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
kuanzia Jumatano, Septemba 9, mwaka huu, 2015.Kabla ya uteuzi wake, Dkt. Tulia
Ackson ni Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
14
Septemba, 2015
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment