WAZIRI
Mkuu Mizengo Pinda amesema atalimaliza tatizo la maji katika mji mdogo wa Magu
ili kuwaondolea shida hiyo wakazi wake ambao kwa sasa ni asilimia 17 tu
wanaopata maji safi.
Akihutubia
mkutano wa hadhara mjini Magu katika siku yake ya pili ya ziara ya wiki moja ya
mkoa wa Mwanza leo (Alhamisi Sept. 13, 2012) alisema yuko radhi kufanya
kila atakaloliweza ili tatizo la maji Magu linamalizwa.
“Sitaki
nirudi hapa mnambie kwamba ahh… nawe kumbe ni bomu tu…mimi sikubali kuitwa
bomu. Nikirudi Dar es Salaam kazi yangu ni moja tu, maji ya Magu,” aliuambia
umati wa wananchi waliokuwa wanamsikiliza.
Alisema,
kwanza atafanya kila njia kupata Sh. Milioni 200 kwa ajili ya kurekebisha
mifumo ya maji ili angalau asilimia 30 ya watu wapatao 38,000 (watu 11,400) wa
mji wa Magu wapate maji.
Pili
amewaagiza wataalamu kufanya mchanganuo wa kuboresha mfumo wa maji
utakaogharibu Sh. Bilioni 8, ili fedha hizo zipatikane awamu kwa awamu na
baadaye asilimia 70 ya wakazi hao (watu wapatao 27,000) wapate maji
safi, alisema.
Maji
safi ni kilio cha wakazi wa mji wa Magu unaokua kwa kasi, ambao uko karibu na
Ziwa Victoria. Mahitaji halisi ya maji mjini Magu ni mita za
ujazo zaidi ya 7,000 kwa siku, lakini uzalishaji sasa ni mita za ujazo 1,200
tu.
ATOA SH. MILIONI 15 KWA VIKUNDI VYA VIJANA WATAKAOCHONGEWA
MITUMBWI KWA MPANGO WA “KOPA MTUMBWI LIPA MTUMBWI”
Alisema
aatamkabidhi fedha hizo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Injinia Evarist Ndikilio, ili
vijana watakaojiunga katika vikundi watapatiwa mtumbwi, lakini watalipa mtumbwi
ili mpango huo uwe endelevu. Mtumbwi mmoja unagharimu Sh. 300,000/= na kwa
fedha hizo itapatikana mitumbwi 50.
Waziri
Mkuu aliyasema hayo baada ya kuzindua rasmi gati la kupokelea samaki katika
kijiji cha Kigangama ambako aliambia baadhi ya vijana wanaishia kuajiriwa na
watu wengine kuvua kwa vile wao hawana mitumbwi.
Mapema
alikagua shamba la kilimo cha kisasa cha mboga cha umwagiliaji kinachoendeshwa
na mjasiriliamali mzalendo, Nd. Peter Ngongo Seke, katika kijiji cha Nsola.
Waziri
Mkuu alitembelea shamba hilo la Ngongo Seke Horticulture Farm, ambalo
tayari linazalisha nyanya, matango na pilipili hoho zinazouzwa kwenye migahawa
ya machimbo ya madini ya wawekezaji wakubwa pamoja na maduka makubwa (supermarkets)
Mwanza na Dar es Salaam.
Kilimo
hicho kinaendeshwa kitaalamu, kwa kutumia mbolea asilia, bila ya kemikali na
kwa umwagiliaji wa teknolojia ya matone, ndani ya mabanda maalum. Kwa kawaida,
mboga zinazolimwa kwa mtindo huo huwa zinaagizwa kutoka nje.
Mhe.
Pinda alivutiwa sana na shughuli hiyo na kusema angetaka mashamba ya aina hiyo
yawe mengi katika wilaya ya Magu, katika Mkoa wa Mwanza na nchini kote.
Waziri
Mkuu alikagua mradi wa ufugaji nyuki kisasa na alimtembelea Mwalimu Mbeba,
ambaye aliwahi kumfudisha shuleni zamani.
Kesho
(Ijumaa Sept. 14, 2012) anaitembelea Wilaya ya Kwimba.
(mwisho)
Imetolewa
na:
Ofisi ya Waziri Mkuu,
S.L.P. 3021,
DAR ES SALAAM
Alhamisi
Sept. 13, 2012
No comments:
Post a Comment