Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Peter Kayanda Mizengo
Pinda (Mtoto wa Mkulima) leo Alasiri ya Jumanne tarehe 16 Oktoba, 2012
anatarajiwa kuunguruma Jijini London katika mkutano wake na Watanzania waishio
hapa Uingereza.
Mheshimiwa Pinda ambaye yuko katika ziara fupi ya kibinafsi
hapa London amerudia utaratibu wa kupenda kusemezana na Watanzania hata
anapokuwa kwenye itifaki ya ziara fupi na ya binafsi, tabia ambayo imekuwa
ikisifiwa na watanzania waishio nje ya nchi. Aidha mkutano huu ni wa kwanza kwa
Mheshimiwa Pinda hapa London tangu jaribio liloongozwa na wabunge wa Upinzani
na wachache wa CCM kutaka kumng’oa madarakani liliposhindwa vibaya kwa kupata
saini 70 tu kati ya 357 kupinga Ufisadi uliokithiri miongoni mwa watumishi
vigogo ndani ya Serikali. Mkutano huu wa Waziri Mkuu unakuja katika kipindi
ambacho Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania (CHADEMA) kimebadili ghafla mtazamo
wake kwa watanzania nje ya nchi na kuanza kufungua utitiri wa matawi, kumwaga
Ruzuku na kufanya ziara ya mara kwa mara kwenye matawi yao ili kuwapika makada
wake kwa ajili ya uchaguzi wa 2015. Waziri kivuli wa Mambo ya Nje (CDM) Mhe.
Dibogo Wenje ndiyo kwanza amemaliza ziara yake hapa London akiwa ameacha ahadi
lukuki kwa wafuasi wao akiwataka wajiandae kushika majimbo ya Ubunge na
nyadhifa mbalimbali serikalini kunako baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015. Awali,
tofauti na CCM, CHADEMA walipinga sana uhusishwaji wa watanzania nje ya nchi
katika miradi ya kisiasa na maendeleo ya kitaifa. Katika hoja za msingi, Waziri
Mkuu Pinda anategemewa kuainisha bayana msimamo wa serikali na hatua madhubuti
ambazo imezichukua kutafsiri kwa vitendo Sera na Ahadi ya Chama cha Mapinduzi
ya kujumuisha suala la Uraia Pacha katika marekebisho mapya ya katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa uwakilishi wake wa awali
ulipokelewa kwa hofu miongoni mwa wabunge, baadhi ya wananchi, wanahabari na
wafinyanzi wa Sera katika chelezo mbalimbali za kijamii. Mashauri mengine
yanayotarajiwa katika mkutano huu ni pamoja na maombi ya awali ya CCM UK ya
kutaka Serikali iandae utaratibu maalum wa kuwasaidia watanzania waishiao nje
ya nchi kupata na kuwekeza katika hazina ya ardhi nchini Tanzania kuliko ugumu
uliopo sasa hivi. Aidha Serikali kuhamasisha sekta binafsi za kifedha na mitaji
ya jamii kuwafikia watanzania ughaibuni ili kuhamisha teknolojia, ubunifu na
uwezo wa kuwekeza katika maeneo kama Kilimo Kwanza na Ujasiria mali wa mizania
ya kati. Pamoja na mahudhurio kutarajiwa kuwa makubwa lakini watanzania wengi
wanasemezana kuwa na imani na CCM lakini wanahisi Serikali na mamlaka zake bado
hazija chukua hatua madhubuti kupunguza ufisadi katika utekelezaji wa miradi ya
maendeleo ya kitaifa. Na Clement Mbawala Tanzania Now: Freelance Observers
Slough. St.Marys Road. SL3
No comments:
Post a Comment