Akizungumza katika mahojiano
maalumu kijijini kwake Ibula, katika kata ya Kiwira, wilayani Rungwe,
Mama mzazi wa Marehemu, Esther Mwambenja, alisema kabla ya tukio hilo kutokea kulikuwa na
viashiria vingi vya mumewe kufanya ukatili.
Alisema tukio la mzazi
mwenza huyo kumwiba mtoto na kwenda kumfanyia ukatili huo wa
kinyama lilikuwa la pili, baada ya awali kumuiba akiwa na miaka miwili na miezi
mine na alimrudisha kwa maandishi ya serikali ya kijiji.
Alisema katika tukio la
kwanza la mtalaka wake huyo kumuiba mtoto wao huyo, lilitokea Septemba mwaka
2012, baada ya wiki chache za kumfukuza katika nyumba waliyokuwa wakiishi
katika kitongoji cha Iponjola, kijiji cha Asenga, nyumba iliyotumika kuzikwa
mtoto huyo.
Alitaja sababu za yeye
kufukuzwa ni ugomvi uliotokana na yeye kuhoji sababu za kuficha fedha
kiasi cha sh. 120,000 zilizotokana na wao kwa pamoja kufanya kazi
ya kibarua katika mashamba kijijini hapo na baada ya malipo kutolewa mtalaka
wake huyo alionesha kiasi kidogo cha sh.80,000.
Alisema ugomvi huo ndio
ulisababisha yeye arudishwe kwa wazazi wake, lakini baada ya muda mfupi
mwanaume huyo alimfuata na kumbembeleza ili warudiane na alipogoma
aling’ang’ania aondoke na mtoto .
“Nakumbuka ilikuwa Novemba
mwaka jana baada ya mimi kuondoka nyumbani kwake na kurudi kuishi hapa
nyumbani, siku hiyo tukiwa shambani huyo bwana alikuja hapa nyumbani na kumkuta
mwanangu wa kwanza (Neema Steven ) niliyezaa na mwanaume mwingine” alisema
Mwambenja.
Alisema baada ya kufika eneo hilo majira ya saa mbili
asubuhi alitumia ujanja na kufanikiwa kumuiba mtoto na kisha kutokomea naye
kijijini kwao Asenga, hali ambayo ilisababisha kutoa taarifa kituo cha polisi
Kiwira.
“Unajua kuwa baada ya kwenda
kutoa taarifa polisi walitusaidia kufika kijijini kwao ambapo serikali ya
kijiji ilikubali nimchukue mwanangu kwa kuwekeana mkataba wa kisheria kwa
mujibu wa sheria, kwani alikuwa chini ya miaka saba”.
Aliongeza kuwa Novemba
15 mwaka 2012 serikali ya kijiji chini ya Mwenyekiti, Lutengano Mwakyoma na
mashahidi watano wakiwemo wazazi na ndugu zake, walinikabidhi barua ya kuridhia
kuondoka na mwanangu, huku ikimuonya mume wangu kutorudia kosa hili la kumuiba
mtoto hadi hapo atakafikisha miaka saba.
No comments:
Post a Comment