Marekani imepeleka mitambo ya
kukinga makombora katika kisiwa cha Guam katika bahari ya Pacific huku Korea
Kaskazini ikitishia kurusha makombora ya nuklia nchini humo.
Idara ya ulinzi ya nchi hiyo imesema
kuwa mitambo hiyo itakuwa tayari katika kipindi cha wiki kadhaa , na kuongeza
kwa zana za kivita ambazo zilipelekwa katika eneo hilo.
Korea Kaskazini ilitaja kisiwa cha
Guam kuwa miongoni mwa maeneo yanayolengwa kwa mashambulizi ikiwemo Hawaii na
Marekani.
Korea Kaskazini haidhaniwi kuwa na
teknolojia ya kutosha kushambulia Marekani kwa zana za nuklia au makombora ya
masafa marefu.
Korea Kaskazini inasema kwamba
imewaweka wanajeshi wake, tayari kwa shambulio dhidi ya Marekani ikiwemo
kutumia zana za nyukilia.
Taarifa hii imejiri wakati Marekani
imeimarisha mitambo yake ya kukinga makombora katika kisiwa cha Guam kilichoko
bahari ya Pacific.
Idara ya ulinzi ya Korea Kaskazini
imesema inatoa taarifa kwa Marekani kwamba jeshi lipo tayari kushambulia bila
huruma, kile imetaja kama vitisho vya Marekani dhidi yake.
Utawala wa Pyongyang ulionekana
kukerwa na hatua ya Marekani ya hivi maajuzi ambapo wanajeshi wake walifanya
mafunzo ya pamoja na ambayo yalihusisha utumizi wa zana za kivita.
Hata hivyo wachanganuzi wamesema
Korea Kaskazini haina silaha ambazo zinaweza kushambulia ardhi ya Marekani,
japo katika siku za karibuni imefanya majaribio ya makombora ua masafa marefu.
Hapo jana Jumatano, Korea Kaskazini
iliwazuia wafanyikazi wa Korea Kusini kuvuka mpaka kuelekea katika viwanda vya
pamoja vinavyomilikiwa na nchi mbili, na hivyo kukatiza uhusiano uliobaki kati
yake na Kusini.
Baadhi wanaona malumbano ya sasa
kama hatua ya Korea Kaskazini kushinikiza Marekani kuanzisha mazungumzo ya
pamoja ambayo yataafikia mkataba wa amani.
No comments:
Post a Comment