Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amewaondoa katika
nyadhifa zao, Wakurugenzi mbalimbali kwa sababu zilizoelezwa kushindwa
kutekeleza majukumu yao.
Hatua ya Nyalandu imekuja ikiwa ni utekelezaji wa azimio la Bunge
la Desemba 22, 2013 lililotaka Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kuwajibishwa
kutokana na tuhuma za uzembe na ukiukwaji wa haki za binadamu katika Operesheni
Tokomeza.
Nyalandu alisema: "Namwondoa Prof Alexander Songorwa
(Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori) na kumteua Paul Sarakikya kukaimu nafasi
hiyo."
Alisema pia kuwa amemwondoa Mkurugenzi Msaidizi wa Matumizi
Endelevu ya Wanyamapori, Profesa Jafari Kidegesho kwenye nafasi hiyo na Dk
Charles Mulokozi ameteuliwa kushika wadhifa huo.
Mwingine aliyeteuliwa ni Julius Kibebe kuwa Mkurugenzi Msaidizi
Uzuiaji-Ujangili, nafasi iliyoachwa wazi na Sarakikya wakati Mkurugenzi
Msaidizi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu, Nebbo Mwina anabaki kwenye nafasi
yake.
Nyalandu alisema Herman Keiraryo anaendelea kuwa Mkurugenzi
Msaidizi wa Uendelezaji wa Wanyamapori na kwamba waliotangazwa kuondolewa
kwenye nyadhifa, kazi zao mbadala zitatangazwa baadaye.
Waziri Nyarandu alitoa siku 30 kwa Wakurugenzi Wakuu wa kila
Idara, Shirika na Taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii, kutengeneza viashiria
vya utendaji kazi (Key Performance Indicators) na kuvikabidhi kwake.
Alisema hatua hiyo itafanikisha kufikiwa malengo ya wizara hiyo,
kwani uwajibikaji na ufanisi wa kazi za kila siku utapimwa katika hali ya uwazi
ili mikakati ya wizara itekelezwe katika mifumo inayopimika na hatimaye kufikia
malengo yaliyokusudiwa.
Waziri huyo aliagiza kila mtumishi akiwamo yeye mwenyewe,
kutekeleza majukumu yaliyopangwa kwa kuzingatia kanuni za mwenendo (code of
conduct), zitakazopendekezwa na kupitishwa na Baraza la Wafanyakazi la wizara
hiyo.
MWANA HARAKATI
No comments:
Post a Comment