Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeeleza
kuwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Machi umeongezeka ikilinganishwa na
mwezi uliopita kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma
mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu
na Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo amesema kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi
Machi 2014 umeongezeka na kufikia asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.0 mwezi
uliopita.
Amesema kuwa kasi ya upandaji
wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Machi 2014 imeongezeka kidogo
ikilinganishwa na ile iliyokuwepo mwezi Februari huku kukiwa na ongezeko
dogo la upandaji wa bei kwenye baadhi ya bidhaa na huduma mwezi huu
ikilinganishwa na bei za mwezi Machi mwaka jana.
Ameeleza kuwa mfumuko wa bei
za bidhaa za vyakula na migahawa kwa mwezi Machi umeongezeka hadi asilimia 7.9
kutoka asilimia 6.9 za mwezi Februari mwaka huu huku badiliko la fahirisi za
bidhaa zisizo za vyakula likipungua hadi asilimia 5.2 kwa mwezi Machi 2014
kutoka asilimia 6.2 za mwezi Februari.
Amefafanua kuwa mwenendo wa bei za
bidhaa za vyakula kama samaki, mbogamboga, ulezi na matunda, ndizi za kupika na
maharage zimeonyesha kuongezeka kwa kiwango kikubwa kwa mwezi Machi
ikilinganishwa na bei za bidhaa hizo kwa mwaka uliopita huku bei za bidhaa
zisizo za vyakula za vitambaa vya suti za wanaume, gharama ya usafi wa nywele
na usafi binafsi, Petroli, mkaa, huduma za matibabu pamoja na tiketi za
kutazama mpira wa miguu ligi kuu zikionyesha ongezeko.
Kwa upande wa mfumuko wa bei
unaopimwa kwa kipimo cha mwezi,ameeleza kuwa kumekuwa na ongezeko dogo kwa
asilimia 0.6 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 1.4 kwa mwezi
Februari mwaka huu, huku fahirisi za bei za taifa zikiongezeka hadi kufikia
149.49 kwa mwezi Machi kutoka 140.93 za mwezi Machi mwaka uliopita huku
fahirisi za zinazopimwa kwa kipimo cha mwezi zikifikia asilimia 149.49 kutoka
148.62 za mwezi uliopita.
Amezitaja bidhaa zilizochangia
ongezeko la fahirisi za bei nchini kuwa ni pamoja na nyanya, viazi
vitamu, matunda, mchele, tambi na kuku wa kisasa ambao wameongezeka kwa
asilimia 1.8.
Aidha kufuatia hali hiyo
ya mfumuko wa bei Bw. Kwesigabo ameeleza kuwa uwezo wa shilingi 100
ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za jamii kwa mwezi
Machi umepungua na kufikia shilingi 66 na senti 90.
“Kupungua kwa thamani ya Shilingi
kunamaanisha kwamba, kama mtu alikuwa na uwezo wa kununua bidhaa kwa Shilingi
100 mwaka jana, basi kwa mwaka huu itampasa aongeze zaidi ili aweze kununua
kitu kama kile kile, kwa mfano badala ya shilingi 100 inabidi atumie shilingi
134”
Kuhusu ulinganifu mfumuko wa
bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki amesema kuwa una mwelekeo
unaofanana na kueleza kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya umepungua kidogo na
kufikia asilimia 6.27 kwa mwezi Machi kutoka asilimia 6.86 za mwezi
Februari, huku Uganda ikiwa na mfumuko wa asilimia 7.1 kwa mwezi
Machi ikilinganishwa na asilimia 6.8 za mwezi uliopita.
( Na. Aron Msigwa/MAELEZO - Dar es salaam)
Na Mwanaharakati.

No comments:
Post a Comment