KUANZIA sasa, shule yoyote mpya
isiyokuwa na maabara ya sayansi na maktaba haitasajiliwa na wala kuruhusiwa
kutoa huduma; Serikali imeagiza.
Kamishna wa Elimu Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Profesa Eustella Bharalusesa amsema hakuna usajili
utakaotolewa kwa shule yoyote mpya bila kutimiza masharti hayo.
Hatua hiyo ya Serikali ni sehemu ya
utekelezaji wa mpango wake wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya elimu
kuwezesha upatikanaji elimu bora na yenye viwango.
Kamishna huyo wa Elimu alisisitiza,
“hii inatokana na agizo la Rais Jakaya Kikwete kwa shule zote mpya zinazojengwa
kuhakikisha masharti haya yanatekelezwa, vinginevyo, shule husika hazitapewa
usajili hata kidogo.”
Kwa mujibu wa Profesa Bharalusesa,
maabara zinapaswa ziwe zimekamilika kwa kuwa na vifaa vyote vinavyohusu masomo
ya Fizikia, Kemia na Bayolojia.
Vile vile kwa upande wa maktaba,
maelekezo ya wizara ni kwamba lazima ziwe zimekamilika kwa ajili ya kuwezesha
utoaji elimu yenye viwango.
Hivi karibuni, vyombo mbalimbali vya
habari, viliripotiwa juu ya baadhi ya shule za serikali mkoani Arusha kushindwa
kuanza muhula mpya wa masomo kutokana kutokidhi masharti ya kuwa na maabara na
maktaba.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, hivi karibuni aliliambia gazeti hili
kwamba yako mabadiliko mengi yanayotarajiwa kufanyika katika sekta ya elimu.
Alisema mipango mbalimbali pamoja na
sera zitaundwa kukidhi mahitaji hayo. Alisema mabadiliko hayo yatajitokeza
kupitia Sera ya Elimu na Mfunzo inayopitiwa.
Kwa mujibu wa Profesa Mchome, kama
mambo yatakwenda vizuri, sera hiyo itakuwa tayari mwakani na itatumika kutatua
kasoro mbalimbali katika sekta ya elimu.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment