MAC PRODUCTION STUDIO'S

MAC PRODUCTION STUDIO'S
KWA MATANGAZO YA BIASHARA REDIONI( 0767-814844)

Monday, 28 April 2014

UHURU WA HABARI KUONDOLEWA KITANZINI

Zaidi ya washiriki 200 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria kwenye matukio ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, inayotarajiawa kuadhimishwa nchini Mei 3, jijini Arusha. 
Meneja wa Maadili na Usuluhishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Allan Lawa (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar es salaam, kuhusu siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari itakayofanyika jijini Arusha.




Bwana Lawa amesema “Sisi kama MCT tumeandaa machapisho matatu ambayo yatazinduliwa siku hiyo yanayogusia hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania 2013, ripoti ya utafiti wa uvunjifu wa uhuru wa habari katika mwaka 2013, na ripoti ya ukiukwaji wa uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Tuna furaha kuwaambia kwamba machapisho yote haya yatapatikana siku hiyo na wote mnakaribishwa kujipatia nakala zenu,” amesema Lawa.
Amesisitiza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kufika katika ofisi za Makao Makuu ya MCT zilizopo jijini Dar es Salaam kuchukua machapisho hayo ili waweze kuyasoma kwa kina na kuweza kutambua haki zao za msingi. 

Alisema pia kwamba muda si mrefu, nakala za machapisho hayo zitasambazwa na kupatikana kwenye vilabu vya vyombo vya habari (Press Club) vya mikoani ili waandishi ambao wako nje ya Dar es Salaam nao waweze kunufaika na machapisho hayo. 

Kati kati ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), Bw. Mohamed Tibanyendera  akizungumza kuhusiana na maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari yatakayofanyika wiki hii duniani kote. 


Bw. Mohamed Tibanyendera, amesema kwamba maadhimisho hayo yenye lengo kuu la kulaani maovu wanayofanyiwa waandishi wa habari barani Afrika na duniani kote, yatafunguliwa na Jaji Mstaafu Mark Bomani.

Tibanyendera amesema kwamba, pamoja na mambo mengine maalum ambayo yatakuwa yameandaliwa, matukio ya mwaka huu yataambatana pia na uzinduzi wa kitabu kiitwacho “Hii Ndiyo Demokrasia, Toleo la 20”, kitachokuwa na taarifa muhimu kuhusu waandishi wa habari walionyanyaswa na kufanyiwa vitendo vilivyokiuka haki za binadamu, barani Afrika. 

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa ambao ni mmoja wa wadhamini wa siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, Bi. Usia Nkhoma Ledama (wa pili kutoka kulia), ambaye alisisitiza kwamba uhuru wa vyombo vya habari nchini ni muhimu kusaidia nchi zinazoendela kufikia malengo ya milenia.


Maadhimisho hayo yanakauli mbiu ya “Uhuru wa vyombo kwa Maendeleo ya Utawala Bora”.
 

Na Mwanaharakati.

No comments: