HATIMAYE ugonjwa wa homa ya
Dengue umeripotiwa kuingia Mkoani Mbeya baada ya kupatikana kwa kesi ya
mgonjwa mmoja mwanamke ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, huku wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kukisikika tetesi za uwepo wagonjwa wa ugonjwa huo ila haijathibishwa.
Mwanamke huyo ambaye ni mkazi wa
Sae, Jijini hapa, ambaye hata hivyo hakuwa tayari jina lake liandikwe
gazetini inasemekana alipata ugonjwa huo baada ya kung’atwa na mbu
aina ya Aides alipokuwa akiishi , Jijini Dar es salaam.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo,
Dk. Gloria Mbwile, alithibitisha kupokelewa kwa mgonjwa huyo na kwamba
tayari hali yake imeimarika baada ya madaktari kumpatia matibabu baada ya
kufikishwa hospitalini hapo.
Amesema mgonjwa huyo alifikishwa
hospitalini hapo Mei 17 majira ya mchana, huku akionesha kuwa
dalili zote za ugonjwa huo
Amesema kutokana na hali hiyo
madaktari walianza kuchukua hatua za haraka kwa kuchukua sampuli za vipimo kwa
ajili ya kuvipeleka Dar es salaam kwa uchunguzi zaidi, wakati huo huo wakimtoa
katika wodi ya wagonjwa mchanganyiko na kumpeleka ile ya binafsi.
Dk. Mbwile amesema hali ya mgonjwa
huyo imeimarika baada ya kupatiwa matibabu ya kina na kwamba hiyo jana
angeweza kuruhusiwa kutokana hospitalini hapo.
Hata hivyo, Katibu wa afya Mkoa wa
Mbeya, Juliana Mawalla, amewataka wananchi wa mkoa wa Mbeya kutoa hofu juu ya
ugonjwa huo kwani mgonjwa huyo alipata maambukizi hayo akiwa Jijini Dar es
salaam na kwamba tayari serikali imeleta vifaa kwa ajili ya vipimo katika
hospitali ya mkoa na ile ya kanda ya Rufaa Mbeya.
Kwa upande wake Mama mzazi wa
mgonjwa huyo, ambaye naye aliomba jina lake lihifadhiwe, amesema mwanae alifika
Jijini Dar es salaam Mei mosi mwaka huu kwa ajili ya kuhudhuria sherehe ya dada
yake na alikaa huko kwa siku nane.
Dengue ambayo tayari imeshaua watu
watano mpaka sasa , huku wagonjwa zaidi ya 400 wakiwa wamegundulika kuambukizwa
na kupatiwa matibabu ya ugonjwa huu katika mkoa wa Dar es salaam hali ambayo
imeibua hofu kubwa kwa wananchi.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment