Muigizaji mkongwe hapa nchini, Said Ngamba , maarufu
kama mzee Small ameiaga dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya taifa ya
muhimbili. 

Habari za kusikitisha
zilizotufikia hivi zinaarifu kuwa Mwigizaji maarufu na mkongwe katika fani ya
vichekesho nchini Tanzania, Said Ngamba maarufu kwa jina la Mzee Small (59)
amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Mzee Small amefikwa na
umauti majira ya saa 4 za usiku wa Juni 7, 2014 katika Hospitali ya Taifa
Muhumbili.
Mke wa marehemu, Bi Fatuma
Saidi, amethibitisha kuwa Msanii Said Ngamba amefariki kweli.
Bi Said amesema kuwa
marehemu mumewe amefikwa na umauti baada ya hali yake kubadilika jana (Juni 7)
asubuhi na kumbikiza Muhimbili ambako alishinda nae akipatiwa matibabu na
majira ya saa tatu usiku alirudi nyumbani na kumwacha kijana wake akimwangalia
mgonjwa na ilipotimu saa tano usiku kijano huyo alirudi na kusema baba
amefariki.
“Nikweli Mzee Small
amefariki”….yalikuwa ni maneno machache yaliyobenba uchungu mzito kufuatia kifo
cha mumewe.
Mipango ya Mazishi
inafanyika nyumbani kwa marehemu Tabata Mawenzi, Dar es Salaam.
HISTORIA YAKE
Katika historia fupi, Mzee
Small alipata elimu ya msingi katika Shule ya Mingumbi huko Kilwa mkoani Pwani.
Mbali na kuwa mkongwe, Mzee Small kila ulipobahatika kuzungumza naye alikuwa
na kawaida ya kutamba kuwa yeye ndiye msanii wa kwanza kabisa Tanzania
Bara kuchekesha runingani.
Mzee Small alianza sanaa
hiyo yapata miaka 31 iliyopita na alipata kufundishwa na mwigizaji Said Seif
‘Unono’ (ambaye pia kwa sasa ni marehemu).
Mbali na kushiriki sanaa
katika vikundi mbalimbali, Mzee Small wakati wa uhai wake ametumika katika
vikundi vya mashirika kama vile Reli, NASACO na mengine mengi, ambayo kwa sasa
hayajihusishi tena na shughuli hizo.
Mzee Small alianza
kujulikana sana katika fani ya uchekeshaji hasa pale alipoibuka na mchezo
uliojulikana kama 50, 50, 100, na ule wa Mjini Shule uliomwelezea mwanamke wa
kijijini aliyeolewa mjini.
Mbali na kutamba na michezo
hiyo, Mzee Small alikuwa ni mcheshi na mwenye kupenda utani wakati wote,
aliibuka na kichekesho kisemacho Nani Mwenye Haki, ambacho baadaye alikiboresha
zaidi.
Baadaye aliibuka na kitu
kingine kikali kilichokwenda kwa jina la Nani Kama Shule, huku akiwa
amewashirikisha wakali wengine kama King Majuto, Kingwendu na wachekeshaji
wengine wanaotamba kwa sasa Bongo.
Mzee Small alikuwa ndiye
mmiliki wa kundi la sanaa linalojulikana kama
Afro-Dance ambalo alilisajili mwaka 1994 kwenye Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) na kutoa ajira kwa vijana wa mitaani.
Pamoja na kuwa na uzoefu
wa kisanaa, lakini mkongwe huyo hakuwahi kuwa na mpango wa kujiunga na kundi
lingine, ila alichokuwa akifanya ni kurekodi na wasanii wengine alipokuwa
akiitwa kwa makubaliano maalum.
Pia mkali huyo wa
vichekesho enzi za uzima wake na uhai wake alikuwa akijishikiza katika duka
moja Kariakoo la Home Shopping Centre kimatangazo.
Kutokana na vichekesho,
Mzee Small huwa anatania kuwa sanaa ilimpa mke wa ndoa katika televisheni
ambaye ni Bi Chau huku akianisha kuwa mkewe, Bi Fatuma huwa hana tatizo lolote
na Bi Chau kwani anajua kinachoendelea kuwa ni kazi tu.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment