Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia
salamu za pole Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali
Mohamed Shein kufuatia kuuawa kwa mtu
mmoja na wengine sita kujeruhiwa akiwemo mhubiri wa amani ajulikanaye kama
Sheikh Ahmed Haidari Jabir wa Zanzibar, kutokana na kurushwa kwa Bomu katika shughuli ya kidini iliyokuwa
ikifanyika katika eneo la Darajani tarehe 13 Juni,2014, mjini Unguja.
‘Hicho
ni kitendo cha kulaaniwa kwa nguvu zote na watu wote wapenda amani Bara na
Visiwani, ni kitendo cha woga na kisicho na ustaarabu na wala hakikubaliki
katika dunia ya sasa’ Rais amesema na kuongeza kuwa;
‘Hiki
ni kitendo kilichofanywa na watu waoga, wasio na ustaarabu wa aina yeyote ile’. Rais amekemea
na kuwataka watu kuwa wastaarabu, wavumilivu na kuheshimu imani na mitizamo ya
watu wengine hata kama hawakubaliani nao.
Rais amesema amesikitishwa zaidi na watu
hao wasio na ustaarabu ambao wamefanya kitendo hicho cha kihalifu kwenye
shughuli ya kidini ambapo ndipo mahali panapostahili Amani, Uvumilivu na Unyenyekevu
zaidi kwa kuwa ni wakati ambapo binadamu anapofanya mawasiliano na muumba wake.
Rais Kikwete amelitaka Jeshi la Polisi
kuwasaka na kuwafikisha mbele ya vyombo vya haki wale wote waliohusika katika
tukio hilo lisilo la kistaarabu.
Imetolewa na; Ikulu-Dodoma
15 Juni, 2014
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment