MAC PRODUCTION STUDIO'S

MAC PRODUCTION STUDIO'S
KWA MATANGAZO YA BIASHARA REDIONI( 0767-814844)

Wednesday 18 June 2014

WATENDAJI SERIKALI KUFUKUZWA KWA UZEMBE NCHINI KENYA


Idara ya polisi nchini Kenya imefanya mabadiliko ya dharura katika afisi kuu za Kaunti ya Lamu, kutokana na mashambulio yaliyosababisha vifo vya watu 60 wiki hii.
Inspekta mkuu wa polisi nchini Kenya David Kimaiyo amechapisha katika mtandao wa jamii Twitter, maelezo ya wakuu wa polisi katika kaunti hiyo waliofutwa kazi mara moja, wakiwemo makamanda wa polisi.
Afisa mkuu wa kituo cha Polisi, OCS, pia amehamishwa kituo mara moja.

Hatua hii tayari imepokewa kwa hisia tofauti huku wakenya wengi wakielezea kutoridhishwa na adhabu hiyo.
Miongoni mwa walioandika malalamiko yao kwa Bwana Kimaiyo, wamesema kuwa mabadiliko yalistahili kufanyika hadi ngazi ya juu zaidi, baadhi hata wakimtaka yeye mwenyewe kama Inspekta wa polisi kujiuzulu.

Tangu kutokea shambulio la Jumapili usiku katika kijiji cha Mpeketoni, karibu na kisiwa cha Lamu pwani ya Kenya, lawama zimeelekezwa kila upande, huku baadhi wakidai kuwa wanasiasa wamehusika na wengine wakilalamikia utepetevu wa polisi katika kutekeleza majukumu yao.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alihutubia taifa Jumanne akisisitiza kuwa ana imani kuwa mashambulio hayo yalichochewa kisiasa.
Ametoa matamshi hayo licha ya taarifa kutoka kwa kundi la wapiganaji wa kiislamu wa AL shabaab waliodai kuwa wao ndio waliohusika.

Matamshi ya rais Kenyatta yame kejeliwa na wanasiasa wa upinzani nchini humo waliodai kuwa rais huyo hana ufahamu wa yale yanayoendelea nchini mwake.
Seneta kutoka chama kikuu cha upinzani, Moses Wetangula amesema matamshi ya rais sio ya kweli. '' Badala ya kuitisha usaidizi wa wenzetu wenye teknolojia bora, hata tutumie ndege zisizo na rubani kuwalipua huko waliko, tunakaa hapa Nairobi na kudai AL shabaab hawakuhusika.'' Wetangula aliambia bunge la Kenya. '' Huu ni mzaha,'' Aliongeza bwana Wetangula.

Lakini uchunguzi uliofanywa na BBC umeonesha kuwa huenda kuna uzito kwa madai ya rais Kenyatta.

Wakaazi wengi wa Mpeketoni waliozungumza na BBC wametueleza kuwa, wanaamini shambulio la Jumapili usiku linatokana na mzozo wa ardhi kati ya jamii zinazoishi huko.
Wakaazi hao wamesema kuwa Al shabaab wamedakia tu kujigamba kwa yaliotokea huko ila wao wanaamini kuwa ni jambo lililokuwa likitokota kwa muda mrefu.

Na Mwanaharakati.

No comments: