Mimi Dr Cyril August Chami, Mbunge
wa Moshi Vijijini (CCM) napenda kueleza masikitiko yangu kwa taarifa za uzushi
na za kutunga kuwa eti mke wangu asiye na jina amemuua mfanyakazi wetu Mwislamu
kwa sababu "marehemu" alikataa kwenda kanisani.
Mimi sina mfanyakazi wa jina hilo la
Mariamu. Wala sina mfanyakazi mwenye umri wa miaka 16. Hatuna tatizo lolote la
mfanyakazi yeyote kupigwa, achilia mbali kuuawa. Lakini taarifa hizo ambazo ni
za uongo mtupu zimewashtua wengi kwa sababu zimejengwa katika misingi ya chuki
za kidini. Mwandishi alilenga kuifanya jamii iamini kwamba mke wangu ambaye ni
Mkristo anawalazimisha wafanyakazi wetu wasio Wakristu waikane dini yao na kuwa
Wakristo. Alilenga kuibua chuki dhidi ya Waislamu na familia yangu.
Kwa hakika, mikakati hii ya
kuichafua familia yangu inasababishwa na harakati za ubunge Moshi Vijijini
2015. Wapinzani wangu wanajua wazi kuwa hawana hoja ya msingi ya kuwafanya
wapiga kura wasinirudishe kwenye nafasi ya ubunge. Kwenye jukwaa na hata kwenye
medani ya maendeleo wanakwama. Kwa mfano, kabla ya barabara za lami kuanza kujengwa
walisema mimi sina ushawishi wa kuifanya Serikali kuzijenga. Sasa zimejengwa na
zinaendelea kujengwa wanajenga hoja kuwa sihusiki wala Serikali ya CCM
haihusiki, bali ni Benki ya Dunia inajenga!!! Wananchi wanawauliza kwani kabla
ya Dr Chami kuwa mbunge Benki ya Dunia haikuwepo? Wanakosa hoja! Hivyo hivyo
kwa mashule, maji, vyuo vya ufundi nk.
Kwa hiyo kwa upeo wao wanaona silaha
pekee waliyo nayo ni kuzua kashfa dhidi yangu. Miezi michache iliyopita walizua
nimeuza shamba la KNCU kwa shilingi bilioni 4 wakati mimi sina wadhifa wowote
KNCU. Eti nimeuza nyumba mbili za Coffee Curing Moshi wakati mimi sina wadhifa
wowote Coffee Curing. Walipoona tuhuma hizo za kutunga hazijakubalika masikioni
mwa wapiga kura wa Moshi Vijijini, sasa wamezua hili la mke wangu kuua
ili Waislamu wa Moshi Vijijini wanione mtu nisiyefaa.
Sasa mimi napenda kuwauliza maswali
haya:
Huyo mke wangu muuaji anaitwa nani?
Inaingia akilini kweli kwamba mke huyo muuaji hafahamiki jina kwa hao
"majirani" wetu wa kufikirika? Binti Mariamu kauawa mji upi? Kwa nini
majirani hao wenye uchungu hawajatoa taarifa kwa RPC wa mkoa au kanda husika?
Maiti kahifadhiwa hospitali ipi? Au "mke" wangu amekaa naye ndani
baada ya kumuua na majirani wamekaa kimya tu?
Kwa desturi za dini ya Kiislamu binti
huyo angeshazikwa sasa maana kwa mujibu wa habari hiyo ya kizushi,
"aliuawa" usiku wa kuamkia jana. Je, kazikwa makaburi yapi na yako
mji gani? Nani kahudhuria hayo mazishi? Kwa nini vyombo vya habari
visituonyeshe hayo mazishi? Kwa nini RPC mhusika asimkamate huyo mke wa mbunge
fedhuli namna hiyo na muuaji asiyevumilika?
Kwa nini polisi hawajaniita mimi Dr
Chami kunihoji kuhusu huyo "mke" wangu? Si wanajua niko jimboni Moshi
Vijijini na RPC Boaz wa Kilimanjaro anafahamu niko jimboni, tena jana nimeutembelea
msikiti mmoja kwa minajili ya kuutafutia umeme na maji? Sote tunafahamu kuwa
kuna mkuu mmoja wa mkoa alimuua mtu kwa kumpiga risasi na alikamatwa akapelekwa
mahabusu. Huyo mke wa Dr Chami ni maarufu kuliko Mkuu wa Mkoa? Kwa nini
asikamatwe tuione sura yake magazetini?
Majibu ya maswali haya HAYAPO kwa
sababu kila kitu kimetungwa kwa kujenga chuki tu. Hakuna Mariamu, hakuna
kipigo, hakuna kifo. Ila kuna UBUNGE WA MOSHI VIJIJINI. Ndio unaopiganiwa,
hamna kingine. Napenda kuwaasa wanasiasa wenzangu kuwa Watanzania wa leo
si wa jana. Si jambo rahisi kuwaghilibu kwa staili hii. Waende kwa wananchi
wachape kazi. Wasipofanya hayo wakadhani uongo wa mitandao utawapa ubunge
watashangazwa mwaka kesho 2015.
Mimi naendelea kuwaahidi wapiga kura
wangu utumishi wa dhati. Nawapa pole ndugu zangu wa Kiislamu kwa usumbufu
walioupata. Waislamu wa Moshi Vijijini wananifahamu kama kiongozi nisiyewabagua
kwa sababu ya dini yao. Wanafahamu kuwa nawapenda na nafahamu kuwa wananipenda
sana. Ndiyo maana wengi wamejiuliza iweje tena mke wangu amwage damu ya
Mwislamu kwa sababu iliyotajwa. Naendelea kuwaahidi Waislamu wote upendo na
ushirikiano siku zangu zote za kuwatumikia.
Wasalaam
Dr Chami.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment