WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema
Serikali inaandaa kongamano la siku mbili litakalojadili mustakabali wa wana
diaspora wa Tanzania kutoka nchi zote duniani ikiwa ni pamoja na kuwakutanisha
na makampuni na wafanyabishara mbalimbali.
Ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki
wakati alipokutana na Watanzania wanaoishi Uingereza kwenye mkutano uliofanyika
ubalozi wa Tanzania jijini London.
Waziri Mkuu alisema kongamano hilo
ambalo limepangwa kufanyika Agosti 14-15, mwaka huu, linalenga kuitambulisha
rasmi diaspora ama jamii ya Watanzania inayoishi ughaibuni kama wadau muhimu
katika kuleta maendeleo nchini Tanzania. "Lengo letu hasa ni kutaka jamii
ya Watanzania ielewe kwamba tunao Watanzania walioko nje ya nchi kwa maelfu na
kuna sehemu mnaweza kuchangia katika maendeleo ya nchi," alisema.
Mbali na hilo, Waziri Mkuu
alisema, katika kuitambua rasmi jamii ya wanadiaspora, Serikali itapenda kujua
wako, ni wangapi na wanafanya nini ambacho kama Serikali itahitaji
ujuzi/utaalamu wao, inaweza kuwapata wapi.
Alisema kongamano
hilo limeandaliwa kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Umoja wa Wanadiaspora
waliorudi nchini waitwao Tanzania Diaspora Initiative (TDI).
“Kongamano
hilo litasaidia wanadiaspora kuweza kuona fursa mbalimbali zilizopo nchini,
kuvutia wawekezaji wageni kuwekeza Tanzania, kukuza utalii nchini, kuelimisha
jamii juu ya umuhimu wa Diaspora pamoja na kuunganisha wawekezaji wa Tanzania
na wawekezaji walioko nje ya nchi.”
Mada kuu ya
kongamano hilo ni “Connect, Engage, Inform and Invest” na kaulimbiu yake
ni “Nyumbani ni Nyumbani”. Aliwataka wajitokeze kwa wingi
kushiriki kongamano hilo ambalo alisema limeandaliwa mahsusi kwa ajili yao na
wasipojitokeza kwa wingi halitakuwa na maana.
Akifafanua zaidi kuhusu taswira
nzima ya Diaspora, Waziri Mkuu alisema: "Sensa ya mwaka 2012 inaonyesha
katika kaya zote zilizohesabiwa Tanzania Bara kuna mtu mmoja au zaidi ambaye
yuko nje ya nchi. Hii ni sawa na asilimia 1.2. Kwa upande wa Zanzibar, hali iko
tofauti sana. Wao ni mara mbili zaidi yaani kila kaya moja ina watu wawili na
zaidi ambao wako nje ya nchi".
Alisema katika matokeo hayo ya
sensa, ilibainika kwamba wanadiaspora wanaotoka kwenye kaya za mikoa ya
Tanzania Bara wako 116,670 wakati wanatoka Zanzibar wanafikia 304,786. “Idadi
ya Watanzania walioko Diaspora ni 421,456 ni karibu sawa na nusu milioni. Idadi
hii si ndogo, ni kubwa. Na kama kundi hili lingetumika vizuri, fedha
waliyonayo ambayo wanaituma kutoka nje, ingesaidia sana kuendeleza Taifa
letu,” alisema Waziri Mkuu.
Alitumia fursa hiyo kuwaelezea
kuhusu mchakato wa katiba ulivyoenda na ulipofikia, maandalizi ya uchaguzi wa
serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu. “Kama Serikali tunajiandaa kwa
lolote litakaloamuliwa na Bunge Maalum la Katiba. Kikubwa tunachoomba ni kuwa
na mchakato wa amani hadi uchaguzi mkuu ufike,” aliongeza.
Aliwataka wanadiaspora waendelee
kuiombea nchi ili ipate wagombea wenye kujali maendeleo ya watu kuliko kitu
kingine chochote. “Endeleeni kuiombea nchi yetu ili tupate watu waadilifu, watu
ambao wanajali watu wa hali ya chini na wenye kutaka maendeleo ya nchi kwanza
kuliko vitu vingine (people who are for pro-poor development).
“Endeleeni kuiombea nchi yetu amani,
tuendelee kumuombea Rais Kikwete ili amalize kipindi chake vizuri na akabidhi
kijiti kwa mwingine salama,” alisema.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment