MAC PRODUCTION STUDIO'S

MAC PRODUCTION STUDIO'S
KWA MATANGAZO YA BIASHARA REDIONI( 0767-814844)

Wednesday 27 August 2014

MUHIMU SANA!!!UGONJWA WA KIFUA KIKUU NA UKOMA SASA KUKABILIWA


Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashidi akiwasha moja ya kati ya magari manne. 
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashidi (kulia) akipokea ufunguo wa moja ya gari kutoka kwa mwakilishi wa shirika la GLRA nchini Burchard Rwamtoga (kushoto)

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashidi (kulia) akimkabidhi Mratibu wa huduma za kifua kikuu na ukoma mkoa wa Kigoma Dkt. Deus Leonard (kushoto) moja kati ya magari manne  yaliyokabidhiwa kwa Serikali.


Mikoa ambayo imenufaika na msaada huo ni pamoja na Tanga, Kigoma, na Mikoa ya Kanda Maalum ya Ilala na Kinondoni.

Akipokea msaada huo leo (Jumanne Agosti 26, 2014) Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashidi (Mb) aliwataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia kikamilifu matumizi ya vyombo hivyo vya usafiri kwa kuvilinda na kuvitumia kulingana na malengo yaliyokusudiwa. 

Dkt. Seif alisema kuwa vifaa hivyo vimegawiwa kulingana na mgawanyo wa mikoa iliyoanishwa na Serikali katika Mpango wa Taifa wa kudhibiti ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma.

Dkt. Seif alisema Mpango wa Taifa wa kudhibiti kifua kikuu na ukoma umekuwa na mafanikio ambapo  imeendelea kutoa matibabu kwa wagonjwa wote wa kifua kikuu na ukoma bila malipo katika hospitali na vituo vya huduma za afya vya serikali na binafsi nchini.

Aidha, Dkt. Seif amesema kuwa Tanzania imevuka malengo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kuponyesha asilimia 85 ya wagonjwa wote wa kifua kikuu wanaoanza matibabu kila mwaka.

“Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania imefikia viwango vya asilimia 88 ya kuwahudumia na kuwaponyesha wagonjwa hao ambayo ni zaidi ya kiwango cha WHO” alisema Dkt Seif.

Dkt. Seif amesema kuwa kwa upande wa ugonjwa wa ukoma, Serikali inaendelea kufanya kampeni katika mikoa ya Dar es salaam, Dodoma, Kagera, Lindi, Morogoro, Mwanza, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Tabora na Tanga katika kutoa elimu kwa wananchi namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Dkt. Seif alisema wagonjwa wapya wa ukoma waliogunduliwa mpaka sasa na kupatiwa tiba ni 23,667, na Serikali tayari imetoa jozi 35,000 ya viatu maalumu  kwa wagonjwa hao.

“Mpaka sasa tumeweza kufikia malengo ya kimataifa ya kutokomeza ukoma kwa kuwa chini ya mgonjwa mmoja katika watu 10,000 na kufanya ugonjwa wa ukoma kuwa si tatizo kubwa la kiafya kwa jamii nchini” alisema Dkt Rashid.

Naye mwakilishi wa shirika lisilo la kiserikali la GLRA nchini Burchard Rwamtoga  aliusifu kwa ushirikiano uliodumu kwa miaka 37 baina ya Shirika hilo na Serikali ya Tanzania katika mapambano ya magonjwa ya ukoma na kifua kikuu.

Aidha, Rwamtoga aliongeza kuwa Shirika la GLRA hutoa wastani wa Tsh. Bilioni 1.3 kila mwaka kwa Serikali  na kati ya fedha hizo kiasi cha Tsh.milioni 600 hutumika kwa ajili ya manunuzi ya vifaa vya usafirishaji ikiwemo magari, na pikipiki kwa waratibu wa kifua kikuu na ukoma. 

GLRA mbali na kutoa fedha kwa Serikali pia tunaratibu mpango wa  kuwajengea uwezo wa kiutendaji waratibu wa mikoa ikiwemo kutoa mafunzo nje ya nchi kupitia kituo cha ALERT kilichopo nchini Ethiopia, ambacho hujisihusha na mafunzo ya upasuaji na kutoa visaidizi ikiwamo miguu bandia na baiskeli kwa wagonjwa.

Kwa upande wake Mratibu wa huduma za kifua kikuu na ukoma mkoa wa Ilala Dkt. Mbarouk Seif ameishukuru Serikali kuupatia mkoa huowake gari la wagonjwa na kuahidi kuwa Ofisi yake itahakikisha gari hilo linawafikia na kuwahudumia wagonjwa kwa wakati.

Shirika la GLRA ilianza kusaidia wagonjwa wa ukoma nchini mwaka 1959 na kupata usajili mwaka 1977 ambapo lilianza kushirikiana na Mpango wa Kudhibiti kifua kikuu na ukoma (NTLP) nchini uliopo chini ya Wizara ya Afya na Usatawi wa Jamii.
 

Na Mwanaharakati.

No comments: