*Yadhamiria
kuwasaidia wazee wasiojiweza
|
Baadhi ya wanachama wa KAAT wakiwa
katika picha ya pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali
Iddi (Katikati).
|
Uongozi mpya wa Jumuiya ya Watanzania
waliosoma Korea (KAAT) wamekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi mjini Zanzibar na kutoa ombi rasmi la
kuharakishwa kwa kufunguliwa kwa Ofisi za Kibalozi nchini Korea Kusini.
Wakizungumza mara baada ya kukaribishwa
na Mhe. Balozi Iddi, Rais wa KAAT, Bw. Stephen Katemba alitoa wito kwa Serikali
ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, kufikiria kufungua ubalozi nchi Korea
Kusini kwa kuzingatia umuhimu wa nchi hiyo katika uchumi wa Tanzania.
Bw. Katemba alisema kuwa kufunguliwa kwa
ubalozi huo kutaongeza chachu ya mahusiano ya kibiashara na kindugu baina ya
nchi hizi mbili zenye urafiki wa hali ya juu.
“Tunakosa fursa nyingi za kufanya
biashara na Korea Kusini kwani wengi wa wafanyabiashara wa Korea Kusini
tuliokutana nao nchini humo wanaona usumbufu kufuata huduma za kibalozi nje ya
nchi yao,” alisema Bw. Katemba.
Kwa mujibu wa Bw. Katemba, Korea Kusini
ina soko kubwa kwa bidhaa za Tanzania ikiwemo bidhaa za vyakula na matunda, pia
Tanzania ina fursa kubwa ya kupata ujuzi hasa kwenye eneo la kiteknolojia na
ujenzi.
Kwa upande wake Balozi Iddi, alisema
kuwa Serikali inatambua umuhimu na fursa zilizopo nchini Korea, na kuahidi
kulifanyia kazi ombi hilo.
Wakati huo huo, katika kutimiza wajibu
wa kusaidia wazee na watu wasiojiweza, uongozi mpya wa Jumuiya ya Watanzania
waliosoma Korea (KAAT) upo mbioni kufanyia matengenezo nyumba za kukaa wazee za
Sebuleni, mjini Zanzibar.
Akizungumzia mpango huo, Makamu wa Rais,
KAAT (Zanzibar), Bw. Bukheti Juma amesema “KAAT inatambua mchango mkubwa wa
wazee nchini Tanzania, hivyo katika kuhakikisha wanaishi katika mazingira safi
na salama, KAAT tutafanyia matengenezo baadhi ya majengo yaliyo kwenye hali
mbaya kituoni hapo,” alisema.
Kwa mujibu wa Bw. Juma zoezi hilo
linatarajiwa kufanywa katikati ya mwezi ujao.
Na Saidi Mkabakuli/Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment