Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis
(PICHANI)amekubali kumuondolea sakramenti ya upadri, Raymond Mosha wa Jimbo
Katoliki la Moshi ikiwa ni miaka 20 tangu padri huyo aombe kuachana na daraja
hilo.
Barua ya uamuzi wa Papa Francis ilisomwa juzi katika parokia
na vigango vyote vya Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi katika ibada zilizofanyika
katika makanisa ya jimbo hilo.
Miongoni mwa parokia ambazo barua hiyo ilisomwa ni Karanga
ambako Paroko wake, John Matumaini alitoa tangazo hilo katika ibada zote.
Uamuzi huo ambao ni nadra kutolewa na Papa, unamaanisha kuwa sasa padri huyo
yuko huru kuoa na kuwa na familia.
Hata hivyo, wakati uamuzi huo ukitangazwa rasmi juzi, tayari
Padri Mosha ambaye ni profesa wa falsafa na maadili katika Chuo Kikuu cha
Nelson Mandela Arusha, ana mke na watoto watatu ambao kwa sasa wako vyuo vikuu.
Padri Mosha alisema aliandika barua kuomba kuondolewa daraja
hilo mwaka 1994 kabla ya uamuzi kutolewa juzi.
Katika orodha ya mapadre 185 wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi
iliyopo katika tovuti ya jimbo hilo, jina la Padri Mosha linaonekana likiwa ni
namba 23.
Akizungumzia hatua hiyo, Padri Mosha alisema: “Ninafurahi
kufunguliwa kifugo hiki na hii itanifanya niishi kama Mkristo. Kwa vile
hawajaniondolea sifa ya kutoa huduma kama vile ibada za mazishi, sakramenti ya
mwisho na ubatizo, nitaendelea kutoa kwa wahitaji kwa sababu ninaupenda
ukristo.
“Nashukuru sasa nimekuwa muumini wa kawaida nitaweza kufunga
ndoa kanisani kwa kuwa nilikuwa nimefunga ndoa ya kisheria tu kwa DC.”
Kuhusu kwa nini aliamua kuacha upadri, Profesa Mosha alisema
ni baada ya kufanya kazi hiyo kwa miaka 20 na akaona ipo haja ya kuwa na
familia lakini kanisa lilikuwa haliruhusu.
“Sasa kwa kuwa kanisa haliruhusu mapadri kuoa ndiyo maana
nikaamua kuandika barua ambayo hata hivyo, imechukua muda mrefu kujibiwa na
tayari nina watoto watatu wako chuo kikuu.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment