Serikali wilayani Hai imewaasa wananchi kuachana na
tabia ya unywaji wa pombe uliokithiri ambao unaathiri nguvu kazi pamoja na maendeleo
ya jamii na taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya
Hai Novatus Makunga kufuatia habari iliyochapishwa na gazeti la Habari Leo
toleo Na. 02830 la Ijumaa Septemba mwaka huu yenye kichwa cha habari “Ulevi kwa
wanafunzi wa Hai wamtisha DC”.
“Si kweli, hakuna kitu kama hicho wala hakuna
taarifa za wanafunzi kunywa pombe hizo hali inayopelekea kuwa tishio katika
wilaya yetu” alisema Makunga.
Akiongea kwa njia ya simu kutoka wilayani Hai Makunga
alisema kuwa alichosema wakati wa mazishi ya aliyewahi kuwa Shehe wa mkoa wa
Kilimanjaro Alli Lema alisema wazazi ndio wanaokunywa pombe aina ya gongo na
viroba na sio wanafunzi wa shule za msingi wala sekondari.
Akifafanua juu ya suala hilo, Makunga alisema kuwa wazazi
pamoja na vijana wengi wanaokaa vijiweni wakiowemo madereva wa “bodaboda” ndio
kundi linalosadikiwa kukithiri katika unywaji wa pombe aina ya gongo na viroba
ambavyo vinatishia kuathiri mfumo wa uzazi.
DC Makunga aliongeza kuwa pombe hizo ni kali, sio
salama na hazina kiwango ndio maana zinapelekea kupunguza nguvu za uzazi ambapo
hata Wachungaji wa dini mbalimbali wamesema idadi ya watoto wa ubarikio katika
makanisa yao pia imepungua.
Vilevile wilaya ya nchi nzima inaweza kukosa nguvu
kazi kutokana na vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa kupungua au waliopo kutokuwa
na nguvu ya kufanya kazi inavyopaswa kutokana na hali yao ya unywaji wa pombe
hizo zisizo salama.
Katika kukabiliana na hali hiyo, Makunga alisema
kuwa tayari wilaya yake ipo katika hatua za mwisho kukamilisha sheria sheria
ndogo ndogo inayopiga marufuku unywaji wa pombe wakati wa saa za kazi wilayani
humo.
Makunga alisema kuwa kwa sasa Sheria kuu ya Serikali
kuhusu unywaji pombe ndiyo inayotumika ambapo inabainisha kuwa muda wa kunywa
pombe siku za kazi yaani Jumatatu hadi Ijumaa ni kuanzia saa 9: 00 mchana hadi
saa 4:00 usiku na siku za Jumamosi, Jumapili na siku za siku kuu ni kuanzia saa
6:00 mchana hadi saa 5:00 usiku ambapo atakayebainika kukiuka utaratibu huo
atachukuliwa hatua za kisheria.
Sheria hiyo inataja kuwa anayekunywa pombe saa za kazi
atapelekwa mahakamani na kupigwa faini au kifungo cha miezi sita jela au adhabu
zote kwa pamoja.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment