Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za
Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Abbas Kandoro kuomboleza vifo vya
watu 10 vilivyotokea Mbalizi, Mkoani Mbeya tarehe 29 Agosti, 2014 baada ya basi
dogo la abiria aina ya Toyota Hiace maarufu kama Daladala Na. T 237 BFB kugongana
na lori aina ya Tata Na. T 158 CSV. Katika ajali hiyo, watu saba wengine walijeruhiwa
na kukimbizwa hospitali kwa matibabu.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na
taarifa za vifo vya watu 10 na wengine saba kujeruhiwa katika ajali hii iliyotokea
siku chache baada ya ajali nyingine kutokea Mkoani Tabora iliyoua watu 19 na
wengine 81 kujeruhiwa”, amesema
Rais katika salamu zake.
Rais Kikwete amesema
mfululizo wa ajali hizi unaonyesha dhahiri kuendelea kuwepo kwa tatizo la
ukosefu wa umakini miongoni mwa madereva, hivyo jitihada zaidi zinatakiwa
kufanywa kusimamia kikamilifu Sheria ya Usalama Barabarani na kufuatiliwa kwa
karibu kwa mienendo ya wanaoendesha vyombo vya moto, ili ajali hizi ziweze kupunguzwa
na hata kudhibitiwa kabisa katika barabara zetu.
“Naomba upokee salamu zangu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kutokana na ajali
hiyo, na kupitia kwako naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa wafiwa wote
kwa kupotelewa ghafla na wapendwa wao”Ameongeza.
Rais Kikwete amesema
anatambua machungu waliyo nayo wanafamilia, ndugu na jamaa wa watu waliopoteza
maisha yao kwenye ajali hiyo, lakini anawaomba wote wawe wavumilivu na wenye subira
wakati huu wanapoomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao.
“Ninawaombea kwa Mola majeruhi wote wa
ajali hiyo waweze kupona haraka na kurejea katika hali zao za kawaida ili
waweze kuungana tena na familia, ndugu
na jamaa zao”, amemalizia
kusema Rais Kikwete katika salamu zake.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment