Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limefahamishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuwa
Tanzania haitaweza kuwa mwenyeji wa Fainali za Afrika- AFCON 2017 kwa kuwa haijawahi
kuandaa fainali zozote za vijana Afrika. Fainali hizo ni zile za vijana wenye
umri chini ya miaka 17 na 20.
Hivyo, TFF inaelekeza nguvu zote katika kuandaa Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka U17 mwaka 2019.
Tunapenda kuchukua fursa hii kumshukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanazania, Jakaya Kikwete kwa kututia moyo
katika kuomba uenyeji wa AFCON 2017.
Pia tunamshukuru Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara kwa juhudi binafsi
alizozionyesha katika jitihada za Tanzania kuomba uenyeji wa AFCON 2017.
TFF inaamini kwa dhati kuwa uenyeji wa Afrika U17 2019 utaifungulia Tanzania milango ya kuandaa mashindano makubwa zaidi.
WANYARWANDA KUCHEZESHA MECHI YA STARS
Waamuzi kutoka Rwanda ndiyo
watakaochezesha mechi ya Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) kati ya Taifa Stars na Benin itakayofanyika Jumapili (Oktoba 12 mwaka
huu) jijini Dar es Salaam.
Hakizimana Louis ndiye
atakayeongoza waamuzi hao wa FIFA kwa kupuliza filimbi kwenye mechi hiyo itakayochezwa
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 jioni. Atasaidiwa na Simba Honore
na Niyitegeka Jean Bosco.
Mechi hiyo itatanguliwa na
ile ya viongozi wa dini- Kiislamu vs Kikristo kudumumisha upendo, amani na
ushirikiano itakayoanza saa 9 kamili alasiri. Tiketi za elektroniki
zitakazotumika kwa mechi hiyo tayari zimeanza kuuzwa kwa kiingilio cha sh.
4,000 na sh. 10,000.
Wakati huo huo, Kocha Mart
Nooij ameongeza wachezaji watatu kwenye kikosi cha Taifa Stars inayodhaminiwa
na Kilimanjaro Premium Lager ili kukiongezea nguvu kwa ajili ya mechi hiyo.
Wachezaji walioongezwa ni
Jonas Mkude na Joram Mgeveke kutoka timu ya Simba, na Gadiel Michael wa Azam.
MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) litakuwa na mkutano na waandishi wa habari kesho (Oktoba 8 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5
asubuhi kwenye ofisi za TFF, Jengo la PPF Tower.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment