WAZIRI MKUU
Mizengo Pinda amempa miezi miwili Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui,
mkoani Tabora, Bi Khadija Makuani kuhakikisha kuwa watumishi wote wa wilaya
hiyo wanahamia Isikizya yalipo makao makuu ya wilaya hiyo.
![]() |
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatuma Mwasa baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Tabora kwa ziara ya kikazi mkoani humo Oktoba 11, 20-14. |
Ametoa agizo
hilo jana jioni (Jumamosi, Oktoba 11, 2014) wakati akizungumza na mamia ya
wakazi wa Isikizya waliofika kushuhudia uzinduzi wa makao makuu ya polisi ya
wilaya hiyo.
“DED nimekagua
nyumba ya mkuu wa Wilaya na kuzindua nyumba zile nane, miundombinu iliyopo
inatosha, hamia wewe na watu wako. Ninataka ifikapo Desemba 31, mwaka huu wote
muwe Isikizya. Atakayegoma, RC niletee jina lake,” amesema Waziri Mkuu.
“Shauku ya
wananchi kuwasubiri mhamie hapa imetosha. Mtumishi ambaye atagoma ni ishara
kuwa hataki kuwahudumia wananchi, na sisi tutasema hatukutaki. Tatizo la
watumishi wengi ni kujifanya wakubwa mno kuliko wananchi mnaowahudumia,”
alisema huku akishangiliwa na wakazi wa Isikizya.
Waziri Mkuu
ambaye aliwasili mjini Tabora jana mchana, alitembelea makao makuu ya wilaya
hiyo ili kukagua mradi wa ujenzi wa makazi ya watumishi wa wilaya hiyo. Mara
baada ya kuwasili wilayani humo, Waziri Mkuu alizindua nyumba nane za watumishi
zilizojengwa kwa gharama ya sh. milioni 555 ambazo kati yake, sh. milioni 400
ni ruzuku kutoka Serikalini.
Pia alikagua
ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Uyui ambayo iko katika hatua za mwisho za
ujenzi. Kabla ya kuzungumza na wananchi hao, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa
jengo la ghorofa moja la ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ambalo
awamu ya kwanza ya ujenzi itagharimu sh. bilioni 1.1/- na awamu ya pili
itagharimu sh. bilioni 1.4/-.
Alisema
wakati wakisubiri ujenziwa ofisi yao ikamilike, watafute nafasi kwenye ofisi ya
Mkuu wa Wilaya ili waweze kuwa karibu na wananchi na kuwahudumia kutatua
changamoto zinazowakabili.
“Mnakaa Tabora
mjini halafu mnadai mnawatumikia wnanchi wa Uyui. Haiwezekani kabisa. Hayo
mafuta mnayotumia kwenda na kurudi mjini si mngetembelea wananchi wa vijijini
na kuhimiza shughuli za maendeleo?” alihoji.
“Hamieni
hapa muweze kutatua changamoto za wananchi. Kama mngehamia mapema hata tatizo
la maji lingekwishatatuliwa na ujenzi wa nyumba za watumishi wote
ungeshakamilika.”
Kuhusu
changamoto ya uhaba wa maji, Waziri Mkuu aliahidi kuwatafutia sh. milioni 200/-
kutoka wizara husika ili ziwezeshe kuvuta maji kutoka chanzo cha Igombe
kilichopo km. 35 kutoka Isikizya.
Aliwapongeza
askari ambao wameamua kuhamia katika wilaya hiyo na kuishi Isikizya licha ya
mazingira magumu waliyoyakuta. Alisema atawasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi
nchini (IGP) ili waone namba ya kuwasaidia kuapata walau nyumba pacha mbili au
tatu (two in one) zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa wilayani humo.
Alimtaka
pia Mkuu wa Mkoa huo, Bibi Fatma Mwassa aangalie uwezekano wa kuwatumia vijana
waliojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kupata utaalamu wao na
kuuhamishia kwa wananchi. “RC tafuteni namna ya kutumia utaalamu wa hawa vijana
wa JKT ili wawafundishe wananchi mbinu za kilimo bora, ufugaji bora ama ujenzi
wa nyumba bora. Siyo mnawatumia kwa kuimba tu,” alifafanua.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment