MSANII Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ huenda akaingia matatani baada ya juzi kupanda jukwaani kutumbuiza katika Tamasha la Serengeti Fiesta 2014 akiwa amevaa sare ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kinyume cha sheria.
Tangu msanii huyo afanye hivyo, mjadala umeibuka kwa wengi
wao kujiuliza nini maana yake na kama alifanya hivyo kwa kibali maalumu au la,
hasa ikizingatiwa ni hivi karibuni Jeshi hilo lilitoa onyo kwa wasanii na
wengineo kutotumia mavazi hayo.
Mbali ya Diamond, hata vijana wake nao walishambulia jukwaa
wakiwa katika mavazi hayo, akiwemo msanii aliyemshirikisha katika moja ya
nyimbo zake, Ney wa Mitego.
Wakati shoo hiyo ikiendelea, baadhi ya mashabiki walianza
kumzomea kila alipoimba kabla ya video kubwa ambazo zilikuwa mbele ya jukwaa
hilo kuanza kuonyesha picha za mnato na video za mwanamuziki huyo akiwa amevaa
mavazi hayo huku akiwa kama askari ‘anayekoki’ risasi katika katika bastora na
baadaye katika bunduki ya kivita.
Kitendo hicho, kilionekama kuwakera zaidi maelfu ya wapenzi
na mashabiki wa muziki waliokuwa wamejazana katika viwanja vya Leaders Club,
huku kila mmoja akiwa na tafsiri yake.
Baada ya tukio hilo la juzi usiku, kitendo cha nyota huyo
kuvalia mavazi hayo ya JWTZ, kimeibua mjadala hadi katika mitandao ya kijamii
kuanzia jana asubuhi, ambapo picha za msanii huyo zikitumika kujenga hoja ya
uhalali wa kufanya hivyo, huku vijana kadhaa wanaokutwa nazo mitaani wakiteswa
vibaya na jeshi hilo.
Kwa upande wake Diamond, alitoa taarifa ndefu katika ukurasa
wake wa Facebook na Instagram, akiishia kuelezea ni kwa nini alizomewa katika
shoo hiyo.
Tanzania Daima ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kinondoni, Camilius Wambura juu ya kitendo cha msanii huyo, alisema alikuwa
hajui chochote na kuahidi kulifanyia kazi kama atapelekewa taarifa na wasaidizi
wake.
Alipotafutwa Kaimu Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Msanja, simu
yake iliita bila kupokelewa na alipotafutwa msaidizi wake, alikiri kupata
taarifa na kujionea kupitia shoo hiyo, huku akisisitiza bosi wake anaweza
kulizungumzia hilo.
Tukio hilo limefanyika ikiwa ni siku chache tu tangu kijana
mmoja aliyekuwa amevalia mavazi ya kijeshi maeneo ya Kariakoo, jijini Dar es
Salaam, kuvuliwa na kupewa adhabu ya kuogelea katika dimbwi la maji machafu
yaliyotuama.
Aidha, msanii Gwamaka Kaihula ‘Crazy GK’ aliwahi kuhojiwa na
Jeshi hilo kwa kutumia mavazi ya kijeshi katika kibao chake cha Simba wa
Afrika, ambapo alijitetea pamoja na kuomba msamaha kwa kilichofanyika.
Kutokana na wimbi la watu mbalimbali hasa wasanii kuvalia
mavazi yanayofanana na sare za jeshi hilo, hivi karibuni Kurugenzi ya Habari na
Uhusiano Makao Makuu ya JWTZ, ilionya kama ifuatavyo:-
Kumejitokeza kama fasheni kwa baadhi ya wasanii,
hasa wanamuziki wa Bongo fleva, kurekodi video zao wakiwa wamevaa sare za jeshi
kama vile suruali, viatu, fulana, kaptula, mabegi au kofia.
Inawezekana kwa namna moja ama nyingine, baadhi ya watumiaji
wa sare hizo hawafahamu ni kinyume cha sheria ya nchi kukutwa nazo, ingawa
kutokujua sheria bado sio utetezi mbele ya mahakama.
Mtu yeyote yule asiye na ruhusa ya kushona, kuuza au kuingiza
nchini sare za jeshi, atakuwa ametenda kosa, kwa hiyo atafikishwa mahakamani na
kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Katika uvaaji au uingizaji nguo, kama itatokea
kwamba nguo hizo zinafanana kwa aina yoyote ile na zile za Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania, ikadhaniwa kuwa ni hizo, mtu huyo ana hatia na anastahili
kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria zinazohusu sare za
majeshi zilizopo, ilifafanua taarifa hiyo.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment