Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Alhamisi, Oktoba 9, 2014, amekuwa Mgeni
Maalum katika Sherehe za Kuadhimisha Miaka 52 ya Uhuru wa Uganda zilizofanyika
kwenye Viwanja vya Sherehe vya Kololo mjini Kampala.
Kwa nafasi yake ya kuwa Mgeni Maalum,
Rais Kikwete amekuwa kiongozi pekee mwalikwa kupata nafasi ya kutoa salamu kwa
wananchi wa Uganda ambayo Oktoba 9, mwaka 1962, ilipata Uhuru kutoka kwa
wakoloni wa Kiingereza.
Viongozi wengine ambao wameshiriki
katika sherehe hizo za kufana na zilizohudhuriwa na mamia kwa mamia ya wananchi
ni Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Makamu wa Rais
wa Burundi na wawakilishi wa nchi za Kenya na Ethiopia.
Rais Kikwete ambaye aliwasili Uganda
mapema jana asubuhi akitokea Dodoma, ambako juzi alipokea Katiba
Inayopendekezwa katika sherehe kubwa na ya kufana sana iliyofanyika kwenye
Uwanja wa Jamhuri, amekwenda moja kwa moja Uwanja wa Kololo, ambako aliingia
dakika mbili kabla ya kuingia kwa mwenyeji wake, Rais Yoweri Kaguta Museveni.
Akimtambulisha Rais Kikwete kwa wananchi
waliofurika kwenye Uwanja huo wa Kololo, Rais Museveni aliwaambia wananchi hao:
“Hapa mbele yenu mnaona Jeshi imara
kabisa la UPDF (Uganda People’s Defence Army) na Jeshi la Polisi lililo imara
pia. Nguvu na uwezo huu wa Jeshi na Polisi wetu umejengwa na pande mbili
kubwa.”
Ameongeza Rais Museveni: “Upande wa kwanza ni sisi wenyewe wananchi
wa Uganda na hili mnalijua vizuri sana. Upande wa pili alikuwa ni Mwalimu
Julius Nyerere, Mwanzilishi na Baba wa Taifa la Tanzania. Yeye hatunaye tena,
yeye sasa amekuwa Omugenzi, yaani ametangulia, kama sisi sote tutakavyokwenda.
Hata hivyo, leo tunaye mmoja wa viongozi wa
Tanzania ambao wamemfuatia Mwalimu Nyerere katika uongozi wa nchi hiyo, naye ni
Rais Kikwete. Karibu Rais Kikwete uzungumze na wananchi wa Uganda.”
Akizungumza kwa ufupi tu na wananchi
hao, Rais Kikwete amewaambia wananchi hao: “Ndugu
zangu wananchi wa Uganda, nawaleteeni salamu nyingi za kindugu na kirafiki
kutoka kwa ndugu zenu wa Tanzania. Wamenituma niwaletee salamu nyingi za
pongezi katika kuadhimisha miaka 52 ya Uhuru wa nchi yenu.”
Rais Kikwete aliwapongeza wananchi wa
Uganda kwa mafanikio makubwa ambayo yamepatikana tokea Uhuru na hasa katika
miaka 28 ya uongozi wa Rais Museveni.
“Mwenye
macho haambiwi tazama na mwenye masikio haambiwi sikia. Kama kuna mtu haoni
maendeleo dhahiri kabisa ambayo yamepatikana chini ya uongozi wa Rais Museveni
basi ana lake jambo ama hataki tu kuambiwa, kutambua na kukubali ukweli.”
“Chini
ya uongozi imara wa Rais Museveni, Uganda imefanikiwa kurejesha amani na
utulivu, jambo ambalo kuna wakati lilipotea kabisa katika nchi hii
madhubuti. Kwa niaba ya wananchi wa
Tanzania, napenda kukupongeza wewe Mheshimiwa Museveni na wananchi wote wa
Uganda kwa mafanikio haya,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete ambaye amefuatana na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe,
ameondoka Uganda mara baada ya kumalizika kwa sherehe hizo kwenda Mwanza,
ambako atafanya ziara ya siku mbili kukagua shughuli za maendeleo katika mkoa
huo.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment