Rais Jakaya Kikwete amemteua Bw. Seperatus
R. Fella kuwa Katibu wa Sekretarieti ya Kamati ya Kuzuia Biashara Haramu ya
Binadamu.
Kabla ya uteuzi huo, Bw. Fella
alikuwa Kaimu Katibu wa Kamati hiyo na uteuzi wake unaanzia mwezi Agosti, 2014.
Kamati ya Kuzuia Biashara Haramu ya
Binadamu ilianzishwa chini ya Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Binadamu ya
mwaka 2008 na kazi kubwa ya Kamati hii ni kuzuia na kudhibiti biashara haramu
ya usafirishaji wa binadamu.
Chimbuko la kutungwa kwa Sheria ya
Kuzuia Biashara haramu ya Usafirishaji wa Binadamu ni Itifaki ya Kimataifa ya
kuzuia, kupambana na kutoa adhabu kwa watekelezaji wa biashara ya usafirishaji
haramu ya binadamu, hasa wanawake na watoto. Itifaki hii ni nyongeza ya Mkataba
wa Umoja wa Mataifa dhidi ya uhalifu wa kimataifa wa kupangwa, ambapo Serikali
ya Tanzania imeridhia Mkataba huo na itifaki yake.
Juhudi za Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania za kushughulikia biashara haramu ya usafirishaji wa
binadamu zinaendana pia na Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu, Mkataba wa
Kimataifa wa kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya Wanawake na Mkataba wa Haki
za Watoto wa mwaka 1989.
Makosa yanayovunja Sheria ya kuzuia
Usafirishaji haramu wa Binadamu ni pamoja na kupanga, kupangisha au kutumia
nyumba au jengo kwa
ajili ya biashara ya usafirishaji wa
binadamu na kughushi hati za Serikali kwa madhumuni ya kukuza biashara ya
binadamu. Makosa mengine ni kujipatia pesa kwa kuwatumikisha kwa nguvu watu
wazima au watoto wa kike au kiume katika kufanya kazi za ndani au biashara
nyingine haramu kama ngono na usafirishaji na usambazaji wa madawa ya kulevya,
baada ya kuwalaghai au kuwachukua kwa nguvu kutoka katika makazi yao.
Adhabu kwa wanaotiwa hatiani kwa
kuvunja Sheria hii ni kifungo kisichopungua mwaka mmoja (1) au kisichozidi
miaka saba (7) au faini isiyopungua shilingi milioni mbili (2) au kuzidi
milioni 50 au vyote kwa pamoja. Imetolewa na: Isaac J. Nantanga
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment