Serikali imetoa wito kwa Ofisi za
wakuu wa mikoa kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda kwenye mikoa yao
ili kuweza kukuza uchumi wa mikoa husika na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Bw. Paul
Sangawe, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, anayeshughulikia Biashara za
Kimataifa wakati akiongoza timu ya wataalam kutoka ofisi hiyo iliyokuwa
ikifanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali na
sekta binafsi katika mikoa ya Shinyanga, Mara, Simiyu, na Mwanza.
Bw. Sangawe, alisema kuwa Wajibu wa
Serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuwekeza.
Alifafanua kuwa, moja ya vipaumbele katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
ambao utekelezaji wake unaishia 2015/16, ni miundombinu ili kufungulia fursa za
ukuaji wa uchumi.
Aidha, Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano unaofuata kuanzia 2016/17 utalenga katika kuendeleza viwanda.
Hivyo, alitoa rai kwa viongozi katika ngazi za mikoa kuratibu masuala ya
uwekezaji hususan katika viwanda ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa uwekezaji
huo unawanufaisha wananchi wa maeneo husika kwa kuongeza fursa za ajira na
masoko ya bidhaa za kilimo.
“Uwepo wa viwanda hivi unaonyesha
mwenendo na mwelekeo mzuri wa taifa katika kufungua fursa za maendeleo na
kiuchumi kupitia sekta ya viwanda, hivyo basi iwapo jitihada za kuhamasisha
uwekezaji wa viwanda katika kila mkoa zitatiliwa maanani ni dhahiri kuwa fursa
za ajira zitaongezeka na kasi ya ukuaji uchumi itaongezeka” alisema Bw.
Sangawe.
Akizungumza na timu hiyo ya ukaguzi
wa miradi ya maendeleo ilipotembelea na kukagua kiwanda cha kusindika mafuta
kwa kutumia alizeti na mbegu za pamba cha Jielong Holdings Mkoani Shinyanga,
Kaimu Meneja Utawala Bw. Atanas William alisema kuwa mpaka sasa kiwanda hicho
kinaweza kusindika na kuhifadhi lita milioni 2.4 kwa mwezi.
“Kwa sasa upatikanaji wa mali ghafi
ni wakuridhisha kwa sababu bado tunanunua alizeti kutoka kwa wakulima, na mbegu
za pamba katika vinu vya kuchambua pamba (Ginneries). Tuna mpango wa
kuhamasisha na kuwafundisha wakulima njia bora za kilimo na utunzaji wa mazao
ili kujihakikishia upatikanaji wa mali ghafi yenye ubora zaidi” alisema Bw.
Atanas.
Viwanda vingine vilivyotembelewa ni
kiwanda cha Dahong kinachotengeneza nyuzi za pamba na kiwanda cha Xinghua cha
kusindika ngozi mkoani Shinyanga na kiwanda cha nguo cha Mwatex Mkoani Mwanza.
Kiwanda cha Dahong kina uwezo wa kununua tani 12,000 za pamba kwa mwaka na
kuzalisha tani 7 za nyuzi za pamba kwa siku. Kiwanda hiki kimeanza uzalishaji
mwezi Septemba 2014, na nyuzi zote zinazozalishwa zitauzwa nchini China.
Kwa mujibu wa bwana Luke Li, ambaye
ni afisa fedha wa kiwanda hicho, mipango ya baadae ya kiwanda hicho ni
kutengeneza nguo. Bwana Li pia alisema kuwa kuna mpango wa kujenga kinu
cha kuchambua pamba na kutoa mafunzo kwa wakulima ili kuwezesha upatikanaji wa
pamba yenye ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake, Meneja wa kiwanda
cha Xinghua, Bw. Wang, alisema kuwa usindikaji wa ngozi unasuasua
kutokana na upatikanaji hafifu wa malighafi. Wafugaji wanapowekea alama mifugo
na kutoboa ngozi wakati wa kuchinja, wanaathiri sana ubora wa ngozi alisema
meneja huyo. Katika kukabiliana na changamoto hii, mwekezaji huyo ana mpango wa
kujenga machinjio ya kisasa ambayo pia itahusisha usindikaji wa nyama.
Aidha Bw. Sangawe alitoa rai kwa
viongozi wa mikoa inayotoa ngozi kwa wingi kuongeza jitihada za kutoa elimu kwa
wafugaji kuhusu umuhimu wa ubora wa ngozi ili kuhakikisha ngozi inayopatikana
Tanzania inakuwa na thamani ya hali ya juu.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment