Jeshi la Polisi mkoani Simiyu
linawashikilia wanachama tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA
wilayani Meatu wakiongozwa na Mwenyekiti wa mkoa wa chama hicho kwa madai ya
kufanya vurugu na kuharibu mali.
Wanachama hao pamoja na viongozi wao
mbali na kukamatwa na jeshi hilo jana, wamefikishwa mahakamani, katika Mahakama
ya Wilaya ya Meatu Mkoani hapa kujibu tuhuma zinazowakabili.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake, Kamanda wa Polisi mkoani humo Charlse Mkumbo, alisema kuwa
wanachama hao wakiongozwa na viongozi wao walifika katika ofisi ya Mkuu wa
Wilaya hiyo kusikiliza rufaa yao.
Alisema kuwa chama hicho kiliwasilisha rufaa
yao katika ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo, kupinga pingamizi lililowekwa na CCM
juu ya viongozi wao waliochukua fomu kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi
wa Serikali za mtaa ambazo zilielezwa kujazwa kinyume cha taratibu.
Mkumbo
alieleza kuwa katika kesi hiyo wanachama wa chama hicho waliochukua fomu za
kugombea nafasi mbalimbali walijaza neno CDM katika nafasi ya jina la chama,
hali iliyopelekea CCM kupinga kwa madai kuwa hakuna chama kinachoitwa CDM.
Alibainisha kuwa katika kutolewa majibu ya rufaa yao, ambayo yalikuwa
yakitolewa na Katibu tawala wa Wilaya hiyo, wanachama hao wakiongozwa na
viongozi wao wa Wilaya na Mkoa walikusanyika katika ofisi hiyo kusikiliza
majibu hayo. Katika majibu ya rufaa yao walishindwa baada ya kuelezwa kuwa
hakuna chama kinachoitwa CDM, majibu ambayo waliyapinga na kuamua kufanya
vurugu ambapo walivunja kioo cha nyuma cha gari mali ya Mshauri wa mgambo wa
wilaya hiyo.
Alisema kuwa gari hiyo T-159 DRF ambayo ilikuwa katika eneo la
ofisi hiyo, ilivunjwa kwa kurushiwa mawe na wanachama hao wakipinga maamuzi
hayo, ambapo polisi waliwasili na kuwadhibiti. Mkumbo alieleza kuwa Jeshi la
Polisi mkoani humo lilifanya msako kuwatafuta waliosababisha vurugu hizo,
ambapo liliwakamata Allen Mwakipesile (24) Mwenyekiti BAVICHA Meatu pamoja na
Mshuda Wilson Mwenyekiti Chadema Mkoa wa Simiyu.
Wengine ni Joseph Slumu (34), Simon
Wilu (39), Nghili Matula (55), Kulwa Seleman (36), Moses Chenyabu (48), Bundala
Mwigulu (17) pamoja na Mwashi Tunu (23) wote wanachama wa chama hicho.
Hata hivyo Mkuu huyo wa polisi
alieleza kuwa wanachama hao pamoja na viongozi wao, jana wamefikishwa
mahakamani katika Mahakama ya Wilaya ya Meatu kujibu tuhuma zinazowakabili.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment