Serikali
imewataka Watanzania kuwakataa na kuwakemea kwa nguvu zote watu watakaobainika
kuvuruga amani nchini.
Akizungumza
katika sherehe za kuweka wakfu Kanisa la Kiaskofu la Roho Mtakatifu Jimbo la
Kondoa, mkoani Dodoma zilizofanyika jana Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amesema hatua hiyo itasaidia katika
kuiwezesha Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha amani chini ya misingi ya upendo,
umoja na mshikamano ulioasisiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh
Abeid Amani Karume.
"Katika
siku za hivi karibuni, zimeanza kujitokeza dalili mbaya za baadhi ya wenzetu
ndani ya jamii kuanza kuchezea amani tuliyo nayo. Tunaona vitendo vyao, hata
kusikia kauli zao," alidokeza Dkt. Bilal.
Makamu
wa Rais aliwahakikishia waumini hao kuwa serikali inathamini amani na
itaendelea kulinda amani ya Watanzania, kwa gharama yoyote na kamwe haitaruhusu
mtu au kikundi chochote kile, kwa sababu na kisingizio chochote kuchezea na
kuvuruga amani ya Watanzania.
"Tutatumia
nguvu zote kuhakikisha Watanzania wanaendelea kuishi kwa furaha, bila vitisho
vya usalama wa maisha na mali zao. Mkono wa sheria utamwangukia kwa kishindo,
yeyote atakayebainika kuchafua amani ya wananchi wetu. Tutasimamia hili kwa
ujasiri na hatutalegeza kamba," alisema Makamu wa Rais.
Dkt.
Bilal aliwakumbusha viongozi wa dini wa madhehebu yote nchini kuzidi kuliombea
amani Taifa kwani amani ni sharti la kwanza kwa maendeleo ya binadamu na hata
vitabu vitakatifu duniani vinafundisha na kusisitiza amani kwa wanadamu.
"Nchi
yetu imebarikiwa kuwa na amani, utulivu, umoja na mshikamano tangu tupate
uhuru", alisema Dkt. Bilal na kuongeza "baraka hizi haziwafurahishi
baadhi ya wenzetu, wanakesha kutuombea mabaya ili mradi tu, waone tunafarakana.
Watu wa Mungu mna wajibu wa kupiga goti kila siku kuliombea Taifa letu. Amani
ikitoweka hakuna pakukimbilia".
Aidha,
Aliwakumbusha waumini wa dini zote nchini kwamba, kila mtu ana wajibu wa
kuheshimu dini au imani ya mtu mwingine na kusema dini yoyote ya kweli,
haichochei chuki wala vurugu.
"Napenda
nitoe angalizo kwamba, ni marufuku na dhambi kubwa, kwa mtu au kikundi cha
watu, kukashifu imani au dini ya watu wengine," alisema Dkt. Bilal na
kusisitiza kuwa "dini zote ni njia tu tunazotumia wanadamu kwa lengo la
kumuabudu Mwenyezi Mungu. Hivyo tofauti zetu za kuabudu na kiimani, kamwe
zisitugawe".
Ibada
ya kuweka wakfu kanisa hilo iliongozwa na Mhadhama Polycap Pengo na kuhudhuriwa
na Maaskofu kutoka maeneo mbali mbali nchini, waumini na viongozi wa serikali.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment