![]() |
Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya tawala za mikoa na Serikali za mitaa Athuman Mfutakamba (kulia) akizungumza wakati wa majumuisho ya kamati hiyo baada ya ziara ya siku tano mkoani Kigoma |
Katika hali ya kutaka kuweka mambo sawa kwa wafanyabiashara, Kamati ya Bunge ya tawala za mikoa na Serikali za mitaa imeitaka Halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji kuwashirikisha wafanyabishara katika soko la Mwanga mjini Kigoma kuhusiana na ujenzi wa soko la kisasa unaotarajia kufanywa badala ya soko hilo kupewa mtu mmoja na kuwaondoa wafanyabiashara hao.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Athuman Mfutakamba amesema hayo wakati wa majumuisho ya kamati hiyo iliyokuwa ikifanya ziara ya kukagua miradi katika halmashauri za mkoa Kigoma.
Mfutakamba alisema kuwa kutoshirikishwa kwa wafanyabiashara ambao walikuwa kwenye maeneo husika kabla ya kupewa kwa wawekezaji kumekuwa kukizua malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya Serikali yao na kwamba ushirikishwaji wa wafanyabiashara hao kutasaidia kuondoa malalamiko hayo.
Naye mjumbe wa kamati hiyo Moses Machali alisema kuwa kitendo cha eneo la soko kupewa mtu mmoja kufanya uwekezaji mkubwa na wafanyabiashara waliokuwepo kuondolewa kinazua migongano na migogoro isiyo ya lazima baina ya wafanyabishara na mwekezaji huyo na hivyo kuondoa maana nzima ya kuondoa umasikini kwa jamii.
Machali alisema kuwa ni jambo zuri kama mwekezaji akapewa eneo hilo lakini wafanyabiashara waliokuwepo nao wakaungana na kupewa hisa kwenye mradi husika au kupewa mgawanyo wa maeneo kabla ya mradi kuanza jambo ambalo linaweza kuwafanya wafanyabishara hao kutoa ushirikiano mkubwa wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Hata hivyo machali alisema kuwa vitendo vya baadhi ya maeneo ya biashara kama masoko kupewa mtu mmoja na kuwaacha wafanyabishara kunazua minong’ono ya kuwepo kwa vitendo vya rushwa miongozi mwa watendaji wa serikali.
Akitolea ufafanuzi maagizo hayo Meya wa manispaa ya Kigoma Ujiji, Bakari Beji amesema kuwa pamoja na mpango wa ujenzi wa soko la kisasa lakini kumekuwa na ushirikishwaji wa wafanyabiashara wa soko hapo tangu mradi utakapoanza hadi soko hilo litakapoanza kutoa huduma zake tena.
Bw. Beji alisema kuwa tayari vikao baina ya uongozi wa Halmashauri na wafanyabiashara na kati ya Mwekezaji na wafanyabiashara vimefanyika ili kuwekana sawa kuona kila mmoja atakavyonufaika na uwekezaji huo.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment