Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar,
Salum Mwalimu amemsimamisha kazi mjumbe wa kamati ya utendaji ya chama hicho
Wilaya ya Ukerewe, Wilbrod Machemli kwa kushindwa kutimiza wajibu wake, ikiwa
ni pamoja na kutotangaza ujio wa kiongozi huyo.Rungu hilo pia limemkuta katibu
wa Chadema wilaya hiyo, Libelatus Mlebele ambaye amepewa onyo kali.
Akizungumzia hatua hiyo katika mkutano
wa hadhara uliofanyika mjini Nansio jana, Mwalimu ambaye ameanza ziara mkoani
hapa juzi kwa lengo la kuwashukuru wananchi baada ya kukichagua chama hicho
katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, alisema hakuridhishwa na maandalizi
yaliyofanywa na viongozi hao.
Kutokana na hali hiyo, Mwalimu
alimwagiza Mwenyekiti wa wilaya wa chama hicho, Jacobo Munyaga kwa gharama zake
amwandalie mkutano mwingine kabla ya mwisho wa mwezi ujao.
Mwalimu pia alitilia shaka matumizi ya
fedha yaliyotajwa kutumika kutangaza uwepo wa mkutano wake.
Alisema Chadema hakipo tayari kulinda
viongozi wazembe na wasiowajibika na kuwaonya wajumbe wa kamati tendaji hasa
katibu ambaye bado yupo katika uangalizi wa miezi sita kwa maelezo kuwa anaweza
kuondolewa kazini.
Kabla ya kuchukua uamuzi huo, Mwalimu
aliwaita mbele wakazi wanne wa kata za Kakerege, Nansio, Nakatungulu na Kagera
ambao walikiri kutosikia matangazo ya ujio wake.
Hatua hiyo aliichukua baada ya kuwasili
katika Uwanja wa Mongera wa mjini Nansio saa 9:30 alasiri huku kukiwa na idadi
ndogo ya watu ikilinganishwa na ziara zake za nyuma.
Mbali na hilo, pia Mwalimu ametumia
mkutano huo kukemea matumizi mabaya ya fedha za serikali yanayofanywa na
viongozi waandamizi wakati huduma za kijamii zikizidi kuwa mbaya.
Alisema ziara za mara kwa mara za nje
ya nchi zisizo za lazima zinazofanywa na Rais Jakaya Kikwete pamoja na viongozi
wengine hazina tija kwa taifa.
Naye mwenyekiti wa halmashauri ya
wilaya hiyo, Joseph Mkundi akizungumza katika mkutano huo, alisema katika
katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wao wamepata mafanikio makubwa.
Alisema mbali na kusimamia vyema
matumizi ya fedha za serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, pia
halmashauri hiyo imekamilisha mipango ya kununua greda moja la kutengeneza
barabara lenye thamani ya Sh400 milioni hivi karibuni chama hiko kimeluwa
kikipigania kukishinikiza serikali kuwachukulia hatua watuhumiwa wa ufisadi.
Hata
hivyo, alisema mbali ya halmashauri hiyo kupata hati safi ya matumizi ya fedha
za umma pia hivi karibuni huko jijini Nairobi Kenya, Halmashauri hiyo ilipata
tuzo ya kukidhi vigezo vya sheria ya ununuzi ya umma kati ya wilaya 166 za nchi
nzima.
chanzo: gazeti la mwananchi
No comments:
Post a Comment