WENYEVITI wa Kamati za Kudumu za
Bunge, waliopendekezwa kuwajibishwa na Bunge hilo katika sakata la Akaunti ya
Tegeta Escrow, wamejiuzulu nyadhifa zao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam
jana, Spika Anne Makinda aliwaambia waandishi wa habari katika Ofisi ndogo ya
Bunge, waliotaka kujua hatima ya wenyeviti hao, kuwa hawapo tena katika nafasi
zao baada ya kujiuzulu.
“Wenyeviti hao kwa ninavyojua mimi
wamejiuzulu, kama ambavyo azimio lilivyotaka, kama wapo hizo taarifa mimi sina
na sijui kinachoendelea, nawaambia mimi wameshajiuzulu,” alisema Spika Makinda.
Makinda alisema wenyeviti hao, ambao
ni wa Kamati ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, wa Katiba, Sheria na
Utawala William Ngeleja na Andrew Chenge wa Kamati ya Bajeti, hawaendelei tena
na nafasi zao, kupisha viongozi wengine kuchaguliwa ndani ya kamati husika.
Hata hivyo, Makinda alipoulizwa kama
wenyeviti hao kama wamejiuzulu rasmi kwa barua na kama yeye amezipokea lini,
alisema viongozi hao ni wa kamati na hivyo wamewajibika katika kamati zao.
“Mimi ndiye Spika, nasema
wamejiuzulu… msiniulize barua zao wala nini, heshima ya mtu ni kujiuzulu
mwenyewe bwana na wao wamefanya hivyo,” alisema Spika Makinda.
Katika Azimio namba tatu la Bunge
katika majadiliano ya sakata hilo, Bunge lilielekeza kuwa kamati husika za
kudumu za Bunge, zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya mkutano
wa 18 wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa kamati husika za kudumu
za Bunge.
Utekelezaji wa azimio hilo, unakuja
baada ya Serikali kutekeleza maagizo ya Bunge hilo kwa kuwawajibisha baadhi ya
viongozi wake, waliotajwa katika ripoti hiyo.
Chenge ambaye ni Mbunge wa Bariadi
Magharibi (CCM), alitajwa katika ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) kuwa aliwekewa Sh bilioni 1.6 katika akaunti yake binafsi na
Ngejela ambaye ni Mbunge wa Sengerema (CCM) aliingiziwa Sh milioni 40.4 kwenye
akaunti.
Waliingiziwa fedha hizo na mmiliki
wa Kampuni ya VIP Engineering & Marketing, James Rugemalira. Mwambalaswa
ambaye pia ni Mbunge wa Lupa (CCM), ametajwa kuwa alikuwa Makamu Mwenyekiti wa
Bodi ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO), ambayo Bunge liliazimia kuwa wajumbe
wake wote wawajibishwe.
Katika utekelezaji wa maazimio hayo,
Rais Jakaya Kikwete alimtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka kupisha katika nafasi hiyo ili ateuliwe mtu mwingine na
tayari Profesa huyo ameshapisha.
Profesa Tibaijuka aliingiziwa Sh
bilioni 1.6 katika akaunti yake binafsi, kinyume na kanuni za maadili ya
viongozi wa umma.
Rais Kikwete pia alimweka kiporo
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa
tuhuma dhidi yake.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji
Frederick Werema, alishajiuzulu.
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment