Tanzania imekuwa katika vita ngumu ya
kupambana na matatizo mbalimbali yanayoisumbua, yakiwamo ya kiuchumi, kijamii
na hata kisiasa.
Katika baadhi ya nyakati, matatizo hayo
yamegeuka kuwa kikwazo kwenye azma ya kuwapa maendeleo na ustawi wananchi.
Pamoja na matatizo hayo, siku za
karibuni na pengine miaka michache iliyopita, biashara za dawa za kulevya
imegeuka adui anayeichachafya nchi.
Kwa kiasi kikubwa, biashara hii ambayo
inaonekana dhahiri kuwa inahusisha wengi, wakiwamo watu wazima na hata watoto
na wengine vijana wasomi wazuri, imegeuka vita ambayo kama nchi ijihesabu kuwa
imeshindwa kuidhibiti.
Hatuchelei kusema nchi yetu imeshindwa
vita ya kupambana na biashara hii ya dawa za kulevya kutokana na kauli lukuki
za baadhi ya viongozi wetu wa kisiasa wa ngazi mbalimbali pamoja na juhudi
zinazofanyika kuhakikisha biashara hiyo inakomeshwa.
Ipo mifano michache ya jinsi ambavyo
biashara hiyo imekuwa ikiendelea kuisumbua nchi yetu katika siku za karibuni na
hata watu wake, ikisababisha ongezeko la vijana kugeuka watumiaji, wauzaji.
Tumeeleza awali kuwa Tanzania inapigana
vita hii ikiwa kama tayari imeshindwa, hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba baadhi
ya viongozi wamekuwa wakituhumiwa kujihusisha nayo, lakini hawachukuliwi hatua
zozote licha ya kuambiwa kuwa wanajulikana.
Ni bahati mbaya zaidi kuona kauli za
baadhi ya viongozi wetu zikiendelea kusikika, zikiwataja wahusika wa biashara
hii kuwa wanajulikana, lakini kwa nini hawakamatwi?
Bahati mbaya, baadhi ya vijana wetu
ambao ni nguvukazi muhimu ndio watumiaji, wasafirishaji na hata wauzaji wa dawa
hizo, huku baadhi yao wakikamatwa na wengine kuhukumiwa vifungo vya muda mrefu
au kunyongwa nje ya mipaka ya nchi yetu.
Hukumu hizo chache kati yake
zimefahamika, kuripotiwa kwenye vyombo vya habari nchini au nje ya mipaka ya
nchi, lakini zinachafua, kutia doa jina zuri ambalo nchi yetu imejijengea kwa
miaka mingi iliyopita. Inafaa viongozi watuambie, ni kwa nini kama nchi
tumeshindwa kudhibiti biashara hii ya dawa za kulevya kama wahusika
wanajulikana?
Jeshi la Polisi, Kitengo cha Dawa
za Kulevya wametueleza kuwa baadhi ya nyumba za wakubwa ndizo zinazotumika kama
maficho au vichaka vya biashara hii.
Tunawaamini
polisi, walilolisema ni kweli wanawajua wamiliki wa nyumba zile ambao ni
wakubwa, lakini tunawauliza wamewachukulia hatua gani ili maficho au vichaka
hivyo vya dawa kulevya yaondolewe?
Hakuna
shaka, polisi wanaufahamu ukweli wa mtandao huo wa dawa za kulevya, viongozi au
wakubwa waliojenga au kumiliki nyumba hizo, ambao hawaishi ndani yake bali
wamezipangisha kwa wengine ambao wamezigeuza maficho ya biashara ya dawa za
kulevya.
Kama hivyo ndivyo, tunawashauri kuwa
badala ya kulalamika, wachukue hatua kwa mujibu wa Sheria ya Dawa za Kulevya,
ambayo wanaikariri kuwa inawapa mamlaka ya kuwafikisha wahusika kwenye vyombo
vya sheria ambako huchukuliwa hatua zikiwamo za kufungwa maisha au mali zao
kufilisiwa.
Tunawashauri viongozi wetu wa kisiasa,
vyombo vya dola au ulinzi na usalama wachukue hatua kukomesha tatizo hilo.
Tunadhani, kwa kufanya hivyo,
wafanyabiashara wa dawa za kulevya kama ni wapangaji kwenye nyumba hizo za
wakubwa, wabanwe wawataje wahusika ili mtandao huo uvunjwe.
CHANZO;MWANANCHI
CHANZO;MWANANCHI
Na Mwanaharakati.

No comments:
Post a Comment