Balozi wa Algeria ambaye aliyemaliza
muda wake wa utumishi katika Tanzania, Mheshimiwa Tabat Jallouh amewatakia
Watanzania mwaka wa mafanikio, amani na utulivu wa 2015, kwa kadri nchi
inavyopitia katika mabadiliko makubwa ya kisiasa kwa njia ya kura ya maoni ya
Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu.
Mheshimiwa Jallouh alitoa salamu zake
hizo kwa Watanzania Jumatano, Januari 14, 2015, wakati
alipokuwa anaagana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam.
Balozi Jallouh alimwambia Rais Kikwete
kuwa anasikitika kuondoka mapema bila kuwa shuhuda na shahidi wa matukio hayo
muhimu katika historia na uhai wa taifa la Tanzania.
“Nakutakia wewe binafsi, Mheshimiwa Rais
na kupitia kwako, Watanzania wote, mwaka wenye utulivu, mafanikio na amani kwa
kadri nchi inavyopita kipindi cha kutunga Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu. Ni
matukio muhimu sana katika historia na uhai wa taifa la Tanzania,” alisema
Balozi Jallouh, ambaye pia alimtakia Rais Kikwete maisha marefu na shughuli
zenye mafanikio baada ya kustaafu.
Balozi Jallouh ambaye Tanzania ilikuwa
nchi ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara kuitumikia katika utumishi wake wa
kibalozi, amekuwa Balozi wa Algeria katika Tanzania kwa miaka mitano.
Naye Rais Kikwete amemshukuru Balozi
Jallouh kwa kuinua kwa kiwango kikubwa uhusiano wa Tanzania na Algeria. “Tunakushukuru
kwa utumishi wako, tunakushukuru kwa kutuunga mkono, tumekuwa marafiki wa miaka
mingi lakini wewe umetoa mchango wa pekee. Tutakukumbuka daima.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
14 Januari, 2015
Na Mwanaharakati.
No comments:
Post a Comment